Ndugu zangu,
Waziri Muhongo ameusema ukweli wake kule Dodoma.
Nami nimefuatilia sinema hii ya Dodoma, kila inavyoendelea
ndivyo ninavyozidi kuchoka. Ama hakika, tunakokwenda siko,
tuna lazima ya kujipanga upya.
Namsifu Waziri Muhongo kwa ujasiri wake. Amutusaidia sana
kuyajua yale ambayo yangetuchukua muda mrefu kuyajua.
Kwa kusimama kwenye ukweli Waziri Muhungo ameitendea
haki nchi yetu tuliyozaliwa.
Na tulipofikia hapa ni ukweli tu ndio utakaotusaidia kutupa
ahueni ya hali mbaya tuliyonayo kama taifa. Huu si wakati
wa kutanguliza siasa za vyama bali kuitanguliza Nchi yetu
tuliyozaliwa na tunayoipenda. Kutanguliza uzalendo.
Leo tunabaki vinywa wazi kusikia kuwa hata wachungaji,
na wengine wamejiingiza Bungeni, kuwa nao wanawaibia
Watanzania wenzao. Kwamba nao hawatosheki. Wanaiba
huku wakitaja neno la Mungu. Leo hata wale wanaojinadi
kuwa ni watetezi wa wanyonge wameanza kutiliwa mashaka.
Uwezo wao wa kiuchumi unahusianishwa na ' madudu' kama
haya ya Tanesco. Na kuna hata wenye ' kuwafuturisha' wenzao
wenye uwezo kwa fedha walizowaibia wananchi wanyonge.
Hawa hawana cha swaumu bali wanashinda na njaa kwa
dhambi ya wizi wao.
Tuna lazima sasa ya kuamka na kuwabana wezi wetu. Mwizi
ni mwizi tu, hata kama ni mheshimiwa Mbunge.Na ukweli ndio
unaohitajika sasa. Na si nusu ukweli, bali ukweli mzima hata
kama utatugharimu maisha yetu.
Nimepata kusimulia kisa cha kijana aliyehangaika sana
kuusaka ukweli. Katika pitapita zake akaliona duka. Kibao
kimeandikwa dukani ; ” Hapa tunauza ukweli”.
Dukani hapo ukweli unauzwa kwa kilo. Bei ya robo kilo
ya ukweli imeandikwa, vivyo hivyo,bei ya nusu kilo ya ukweli.
Lakini, mwenye duka hakuandika bei ya ukweli mzima,
kwa maana ya kilo nzima ya ukweli.
Kijana yule akauliza; ” Mie nataka ukweli kilo nzima, mbona
hujaandika bei?”
” Alaa, unataka kilo nzima ya ukweli?” Aliuliza mwenye duka.
” Naam” Akajibu kijana yule.
” Basi, zunguka uje ndani nikuambie bei yake”.
Alipoingia ndani dukani, kijana yule akaambiwa;
” Kijana, hatukuandika bei, maana, gharama ya ukweli
mzima ni uhai wako. Je, uko tayari?”
Kijana yule akatimua mbio. Nyuma aliacha vumbi. Hakuwa
tayari kulipa gharama ya ukwelimzima.
Katika Uislamu inasemwa; sema ukweli, hata kama unauma
na kwamba unaweza kupelekea umauti wako.
Hakika, maandiko ya kwenye vitabu vya dini zetu hizi yana ya
kutufundisha.
Na hilo ni Neno langu la Leo.
Maggid Mjengwa,
Sweden.
No comments:
Post a Comment