Tuesday, November 27, 2012

Mkapa atoa ushauri kwa vijana wasomi“Mimi nashangazwa na vijana kukaa vijiweni mnacheza na facebook, twita na mitandao mingine ambayo haina faida kwenu, nawasihi sana muachane na tabia hiyo, jengeni mazoea ya kuingia katika mitandao yenye faida kwenu na mitandao ya kujifunza wakati wote mambo ya dunia,”

RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa, amewaasa vijana kuitumia elimu waliyoipata katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa ajili ya maendeleo yao na jamii kwa ujumla. Mkapa alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia katika mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu cha St John cha Kanisa Anglikana Mjini hapa.
Mkapa alisema ni aibu kwa kijana wa Kitanzania kutumia muda mwingi wa kukaa na kusogoa mambo ambayo hayana msingi na faida kwake na badala yake watumie muda huo katika kufikiria jinsi ya kuitumikia
nchi yao.

Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa
“Mimi nashangazwa na vijana kukaa vijiweni mnacheza na facebook, twita na mitandao mingine ambayo haina faida kwenu, nawasihi sana muachane na tabia hiyo, jengeni mazoea ya kuingia katika mitandao yenye faida kwenu na mitandao ya kujifunza wakati wote mambo ya dunia,” alisisitiza.

Akizungumza na wanachuo wanaoendelea chuoni hapo, aliwataka kujiepusha na migogoro isiyokuwa na maana na kuacha kuwa walalamikaji na badala yake washirikiane na uongozi wa chuo katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.


“Jiepusheni na migomo isiyo na tija wala msitumie udhaifu wa uhaba wa vitabu na maabara kutojisomea bali tumieni vitabu hivyo vilivyopo na maabara iliyopo kujisomea wakati changamoto hiyo ikipatiwa ufumbuzi.” alisema Mkapa.

Akizunguma kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo, Paul Rupia aliueleza mkutano kuwa St John imejipanga vizuri na kuhakikisha kuwa inajipanua katika majengo ili iweze kuongeza idadi ya wanafunzi pamoja na maeneo ya kusomea.

Alisema katika mkakati huo, Chuo kimepata eneo katika Kijiji cha Nala nje kidogo ya Mji wa Dodoma ambapo wamenunua eneo la ukubwa wa ekari 100.Alivitaja vitivo vitakavyoongezwa katika eneo hilo kuwa ni sayansi ya afya, uandishi wa habari,sayansi ya mawasiliano, uhandisi, na sayansi ya kilimo ikiwamo kitivo cha afya.

No comments:

Post a Comment