Friday, January 4, 2013

Mchezo unaoendelea kuhusu gesi ni hatari


KWA zaidi ya wiki moja sasa, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China.

Chimbuko la mjadala huu ni maandamano yaliyofanyika mjini Mtwara Desemba 27, mwaka jana yaliyoratibiwa na baadhi ya Vyama vya Siasa vya Upinzani kuhamasisha wakazi wa mkoa huo wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam.
Awali tulidhani kwamba msingi wa malalamiko ya wananchi wa Mtwara ni kutokuwa na elimu kuhusu kile kinachofanywa na Serikali katika kutekeleza mradi huu ambao iwapo utakamilika utakuwa na manufaa kwa taifa letu.
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo
Ndiyo maana katika tahariri yetu ya Desemba 28 mwaka jana tulitoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za kuwaelimisha wananchi wa Mtwara kwa kuwapa majibu kuhusu hoja zao hasa jinsi watakavyonufaika na rasilimali hiyo.

Hata hivyo, kadri siku zinavyokwenda suala hili limekuwa likichukua sura tofauti kutokana na makundi mbalimbali ya kijamii kujitokeza na kusisitiza kuwaunga mkono wananchi wa Mtwara katika msimamo wao, siyo tu kutaka mradi huo uwanufaishe, bali katika kupinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.

Makundi haya yapo ya wanasiasa wakiwamo wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa vyama vya upinzani, mashirika ya kijamii na makundi mengine ya kijamii kama wazee ambao jana pia walijitokeza hadharani kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi hiyo asilia.

Kwanza tuweke wazi kabisa kuwa siyo vibaya kwa makundi haya au mtu yeyote kuwaunga mkono wananchi wa Mtwara ambao kwa kudai kila wanachodhani ni haki yao hawavunji sheria yoyote ya nchi.

Lakini kwa kuzingatia mwenendo ulivyo tunapaswa kuchukua tahadhari ya hali ya juu. Tahadhari hii inatokana na matamshi yenye mwelekeo wa kusisitiza kwamba gesi ni mali ya wananchi wa Mtwara pekee, kana kwamba wao ndiyo wenye mamlaka ya kuidhibiti, kuisimamia na kuamua ipelekwe wapi.

Hatari zaidi ni pale kauli za aina hii zinapoungwa mkono na wanasiasa na watu wanaoheshimika katika jamii, ambao tunaamini kwamba wangetumia nafasi walizonazo kuwasaidia Wana-Mtwara kupata haki yao kwa maana ya kudai kufahamu jinsi watakavyonufaika na mradi wa gesi na siyo kupinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.

Kwa kuunga mkono ‘vita’ dhidi ya ujenzi wa bomba hilo, tunatengeneza taifa ambalo kila ukanda au mkoa utaanzisha harakati za aina hiyo zenye lengo la kupinga rasilimali zinazopatikana katika eneo lao zisiguswe wala kuwanufaisha watu wengine.


Kama alivyosema Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, rasilimali za taifa zinapaswa kuwanufaisha Watanzania wote bila ubaguzi. Kwa hiyo harakati zozote zenye mwelekeo wa kujenga matabaka kwa misingi ya rasilimali, hazikubaliki kwani hazina afya kwa ustawi na mustakabali wa nchi yetu.

Tunachopaswa kukidai kama Watanzania ni wananchi wote kunufaika na rasilimali zilizopo nchini na siyo wananchi wa ukanda au mkoa fulani kuwa na mamlaka au uwezo wa kuhodhi rasilimali hizo eti kwa sababu tu zinapatikana katika eneo lao.

Kama tulivyosema katika tahariri yetu ya awali kuhusu suala hili, Serikali kwa upande wake inapaswa kuchukua hatua za kuendelea kuwaelimisha wananchi wa Mtwara hasa kuhusu miradi ya kiuchumi na kijamii ambayo wao watanufaika nayo kutokana na mradi wa bomba la gesi.

Katika hatua hii, Serikali isichoke na iwe tayari kujibu maswali na hoja za wakazi wa Mtwara kadri itakavyowezekana ili kutotoa fursa kwa wale ambao wamekuwa wakitumia suala la gesi kwa malengo yenye sura ya kuligawa taifa.

source : http://www.mwananchi.co.tz/uchambuzi/-/1597604/1657432/-/mkw26fz/-/index.html

No comments:

Post a Comment