Wednesday, February 6, 2013

Mbwana Samatta aiongoza Taifa Starz kuipiga Cameroon 1-0 leo

MBWANA Ally Samatta, jioni hii ameibuka shujaa wa taifa, baada ya kuifungia Tanzania, Taifa Stars bao pekee la ushindi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Cameroon Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Samatta akiwakimbiza Wome ana Ekotto
Mshambuliaji huyo wa TP Mazembe ya DRC, alifunga bao hilo baada ya kumchambua kipa wa mabingwa hao wa Olimpiki mwaka 2000, Effala Komguep kufuatia krosi maridadi ya Salum Abubakar 'Sure Boy'.
 
Starz leo
Sama Goal alitumia akili ya hali ya juu kufunga  bao hilo, baada ya kuwekewa ulinzi mkali kwa muda wote wa mchezo, kwani alifanya kama hawanii mpira na ghafla akauchomokea, wakati mabeki wa Simba Wasiofungika, wakidhani kipa wao atauwahi.
 
Cameroon
Aidha, kwa bao hilo tamu, ni sawa na Samatta au Poppa kuwaomba radhi mashabiki kwa kitendo chake cha kususia kambi ya timu iliyokuwa ikijiandaa kucheza na Zambia.
Huu ni ushindi wa tatu mfululizo wa nyumbani kwa Taifa Stars, baada ya awali kuzifunga Kenya Novemba na Zambia Desemba, zote 1-0.
 
Ngassa akidhibitiwa na Ekotto
 Stars ingeweza kuondoka na ushindi mnene leo, iwapo beki Erasto Nyoni angefunga penalti dakika ya 25, lakini kipa Komguep aliipangua. Penalti hiyo ilitolewa na refa Munyemana Hudu wa Rwanda baada ya beki Ngoula kumuangusha Samatta kwenye eneo la hatari.   

Tanzania; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Salum Abubakar, Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Mwinyi Kazimoto / Thomas Ulimwengu na Amri Kiemba.

Cameroon; Effala Komguep,  Benoit Assou Ekotto, Aminou Bouba, Ngoula/Maukon Jean, Nyom Allan, Pierre Wome, Kingue Mpondo, Bedimo Henri/Ashu Glovis, Tchami Herve/Eloundu, Olinga Fabrice/Edoa Charle na Abubakar Vincent/Bakinde Gerard. 

No comments:

Post a Comment