Monday, February 4, 2013

Mwakyembe awasha moto Tazara

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amekutana na wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara), Makao Makuu Dar es Salaam kueleza uamuzi uliofikiwa kuhusu kukithiri kwa changamoto nyingi.

Akiwa ameongozana na Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji wa Zambia, Yamfwa Mukanga, makatibu na watumishi wengine wa ngazi za juu katika mamlaka hiyo, alifika ofisi hizo baada ya kuitisha kikao cha ghafla.

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe. 

Hatua hiyo imefuatia baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Akashambatwa Lewanika kulalamikiwa na wafanyakazi kuhusu kuwepo kwa utawala mbovu na tuhuma za ubadhirifu wa fedha ndani ya uongozi uliopo.

Akizungumza wiki iliyopita katika mkutano huo, Dk Mwakyembe alisema Bodi ya wakurugenzi ya Tazara imeandaa kamati ndogo kwa ajili ya kukagua mahesabu ya shughuli za utendaji ndani ya uongozi wa Tazara hapa nchini.

“Kamati hiyo imeundwa kutoka ndani ya bodi na itaanza kazi Jumatatu kuchunguza uongozi huu, itakaa hapa kwa mwezi mmoja ,ili tuhakikishe tatizo linaanzia wapi, haiwezekani tupelekwe kijinga kijinga tu,” alisema Dk Mwakyembe.

Dk Mwakyembe alisema hatua hiyo itakuwa ni sawa na dawa ya mwarobaini wa kutibu maradhi yote yaliyopo katika ngazi zote za uongozi wa mamlaka hiyo kwa hapa nchini.

“Haiwezekani shughuli zinafanyika kila siku halafu unatuambia Tazara haikopesheki, ukiangali TRL ina matatizo makubwa zaidi ya Tazara lakini wafanyakazi wanalipwa na hakuna ujinga kama huu,” alisema Mwakyembe.

Mwakyembe aliongeza kuwa endapo kamati hiyo haitakamilisha kazi kwa muda uliopangwa, ataomba uongozi wa Tazara, Zambia kumpatia mtu atakayekaimu nafasi ya mkurugenzi aliyepo kwa sasa.

“Sitakuwa tayari tena kukaa naye,hatuwezi kukaa na mtu asiyetufaa na kabla sijaondoka kwenye nafasi yangu nitahakikisha mdudu aliyepo hapa Tanzania tunamwondoa”alisema Mwakyembe.

Bodi mashakani
Akijibu maswali mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi,Dk Mwakyembe alisema mbali na kuahidi kumwondoa mkurungenzi huyo madarakani, pia aliitupia lawama bodi ya wakurugenzi kutotekeleza maagizo mbalimbali wanayoagizwa na Serikali. Dk Mwakyembe alisema bodi hiyo ilishindwa kutekeleza agizo walilokuwa wamepewa ikiwa ni kuwashughulikia maofisa saba wa ngazi za juu katika mamlaka hiyo.

“Bodi yote haifai, haiwezekani mtu ana kesi yuko mahakamani, lakini anaendelea kula mshahara, kama ana makosa kwanini msikae na kuamua kuliko kukaa naye halafu atatutia hasara?  

Dk Mwakyembe alisema mbali na suala hilo kuwa mahakamani, bodi hiyo ilikuwa na mamlaka ya kuchunguza na kujiridhisha juu ya uhalali wa watumishi hao kuendelea na kazi lakini hata hivyo hawakutelekeza hivyo.

No comments:

Post a Comment