Thursday, June 27, 2013

Busara za Kaka Maganga : Mitazamo na Hulka katika Fedha

Ninapotaja habari ya mtu kuwa na fedha isidhaniwe kuwa ninagusia fedha nyingi sana, la hasha! Watu tunatofautiana sana linapokuja suala la mitazamo na hulka zetu katika fedha. Wapo watu ambao akiwa na elfu kumi tu mfukoni lazima ujue kwa maana ataleta vurugu na maujiko kibao.
Mtu mwingine akiwa na hiyo shilingi elfu kumi mfukoni haoni kama ana fedha, isipokuwa anaweza hata kukueleza kuwa “sina fedha kabisa”. Kwa mwingine milioni moja sio fedha wakati kwa mwingine milioni moja ni utajiri!
Kinachofanya mtu mmoja aone kuwa elfu kumi ni fedha na mwingine aone kama si fedha inatokana na mtazamo wanaokuwa nao watu hawa katika fedha. Mtazamo huu hauanzi pale mtu anapoishika hiyo elfu kumi, isipokuwa ni kuwa mtazamo wao ulishajengeka mapema kabla hata ya kushika hiyo fedha.


Tunaposikia kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira; kuna makundi mawili ya watu yanayolitazama hili kwa mitazamo tofauti. Mosi wapo wale wanaosimama upande wa kulalamika na wakitazamia kuhurumiwa. Ni vema wasomaji mkafahamu siri hii: kihisia, fedha ni kama ina masikio, haitaki malalamiko haitaki manung’uniko!
Ukizoea kulalamika na kunung’unika ovyo unaifukuza fedha! Lakini ukichunguza upande wa hawa walalamishi na wanung’unikaji sana; utagundua kuwa wengi wao huamini kuwa kushindwa kwao ikiwemo kiuchumi(kifedha) ni matokeo ya uzembe ama kutokuwajibika kwa wengine.
Kundi la pili ni wale wanaofikiri namna ya kuikabili na kuitatua changamoto hii. Ndani ya kundi hili la pili ndimo wanakopatikana wale wanaoamua kujiajiri lakini ninaowakusudia zaidi hapa ni wale wanaowasaidia wengine kujiajiri. Hawa ni kundi la watu wanaoamua kufanikiwa katikati ya matatizo na changamoto.Ndio maana ukichunguza kwa umakini utabaini kuwa, watu wanaofanikiwa katika jamii zetu katika maeneo mbalimbali (ikiwemo kifedha) huwa wako “bize” na mambo yao, hawana muda wa kulalamika wala kunung’unika ovyo. Wanaofanikiwa mara zote huwa hawawanyooshei vidole watu wengine kutokana na kushindwa kwao. Wanaofanikiwa huamini kuwa wanawajibika kwa sehemu kubwa katika mafanikio yao.
Kwa kuwasaidia wengine kuweza kujiajiri kundi hili hufanikiwa kujipatia fedha. Unapotatua changamoto ama tatizo lolote kiubunifu ni lazima unufaike. Tunatakiwa tufahamu kuwa matajiri wote duniani wameupata utajiri wao kwa kutatua changamoto na matatizo waliyoyabaini miongoni mwa watu. Fedha zinapatikana kwenye matatizo na changamoto.

No comments:

Post a Comment