Thursday, August 8, 2013

Sakata la Madawa JKNIA: Mwakyembe acharuka!

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameionya Kamati ya Nne ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri wa Anga nchini (NCASC) kujiondoa kabla hajaifikia iwapo mzigo wowote wa dawa za kulevya kutoka Tanzania utakamatwa nje ya nchi ukitoka nchini kwa njia ya anga.

Dk Mwakyembe alitoa onyo hilo jana Dar es Salaam wakati akizindua rasmi Kamati hiyo yenye wajumbe 11 na kusisitiza kuwa ina wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege unaimarishwa, ili kudhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini.

“Mimi sidhani suala la kukamatwa kwa dawa za kulevya katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ni dogo,” alisema Dk Mwakyembe na kusisitiza kuwa kashfa ya dawa za kulevya kupitishwa katika uwanja huo, inadhalilisha jina la Baba wa Taifa kitaifa na kimataifa.


Alisema kutowajibika kwa mamlaka zinazohusika na ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege, kumesababisha kuendelea kwa ugaidi wa kimataifa na kusikitishwa na udhaifu unaofanywa na mamlaka hizo hali inayoliletea Taifa fedheha kubwa.

“Sidhani kama mamlaka hizo zinahitaji sheria ili ziwe na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu,” alisema Waziri na kusisitiza kuwa umefika wakati kwa viongozi kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa ili kuleta tija na maendeleo nchini.

Alisema amekuwa akisikia mijadala kuhusu kukamatwa kwa dawa za kulevya, lakini hakuna anayechukuliwa hatua za kisheria kuhusu kashfa hiyo na kuongeza kuwa viongozi wanakataa kuheshimu sheria, hali ambayo alisema inadhalilisha na kushusha hadhi ya viwanja vya ndege nchini.



Baada ya kuzindua Kamati hiyo, Dk Mwakyembe alizuia zawadi zilizoandaliwa kutolewa kwa Kamati inayomaliza muda wake ikiongozwa na Mwenyekiti, Jafari Mpili na kukataa pia kupiga nayo picha ya pamoja badala yake akaomba akutane na Kamati mpya, jana saa nane mchana kujadili kwa kina majukumu.

Awali, katika hutoba yake kwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa NCASC ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Fadhili Manongi, alitaja changamoto kadhaa za kiusalama katika sekta ya anga nchini.

Changamoto hizo ni pamoja na kuchelewa kuridhiwa na Bunge mikataba ya kimataifa inayohusu na usalama wa usafiri wa anga kama vile mkataba wa Beijing na Itifaki ya Mwaka 2010.

Nyingine ni kutojua taratibu za kiusalama na maneno ya kukatisha tamaa kwa maofisa usalama wa viwanja hasa kutoka kwa viongozi waandamizi wa Serikali kwa kauli zao na kutoelewa kanuni za usalama kwa wadau wengi.

Moja ya malengo ya NCASC ni kushauri TCAA hatua za usalama zinazotakiwa katika viwanja vya ndege ili kudhibiti vitisho na ugaidi dhidi ya usafiri wa anga, viwanja na miundombinu yake.

Doa kwa Taifa Juzi katika taraifa yake, Serikali ilisema biashara ya kusafirisha dawa za kulevya imeanza kutia doa taswira ya Watanzania kimataifa. Ilisema uthibitisho ni kwamba katika baadhi ya nchi, kila Mtanzania anayeingia, hivi sasa anachukuliwa kama mshukiwa wa moja kwa moja wa dawa hizo na hivyo kupekuliwa kwa kina.

Serikali ilisema Watanzania waliokamatwa hivi karibuni wakiwa na dawa hizo wamechangia kwa kiwango kikubwa kutoa doa taswira ya nchi. Wiki iliyopita, Mtanzania Jackline Mollel (35), alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Harare, Zimbabwe akidaiwa kuingiza shehena ya dawa za kulevya zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 72.

Kabla ya tukio hilo, Julai, Watanzania wawili, Agnes Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Oliver Tambo, jijini Johannesburg, Afrika Kusini, wakidaiwa kuingiza dawa za kulevya kutoka Tanzania zikiwa na thamani ya mamilioni ya fedha. Walifikishwa mahakamani jijini humo.

Source : HabariLeo

No comments:

Post a Comment