Wednesday, December 25, 2013

James Kisaka afariki dunia

Marehemu Kisaka akiwa hospitalini siku chache zilizopita
KIPA wa zamani wa klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, James Kisaka amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Burhan, Dar es Salaam.
Mdogo wa marehemu, Benny Kisaka ameiambia BIN ZUBEIRY asubuhi hii kwamba, James Kisaka amefariki baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kichwa, macho na miguu kwa muda mrefu.
Benny amesema mwili wa marehemu kwa sasa bado upo hospitali na wanafamilia wanajikusanya kukutana kupanga utaratibu wa mazishi.


Kisaka (wa pili kushoto) akiwa na kikosi cha Simba SC miaka ya 80's

Kisaka mara ya mwisho alikuwa kocha wa makipa wa Simba SC na alifanya kazi hiyo hadi mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu.
Baada ya hapo ndipo alipoanza kusumbuliwa na maradhi hadi hali yake ilivyokuwa mbaya kiasi cha kuaga dunia.



James Kisaka alizaliwa mwaka 1955 mjini Dar es Salaam na alipata elimu yake ya Msingi katika shule ya Oysterbay na baadaye sekondari za Mzizima na Tambaza, Dar es Salaam pia.
Alianza kupata umaarufu wa soka tangu anasoma na haikushangaza aliposajiliwa na Sigara akiwa kijana mdogo chini ya umri wa miaka 20.
Baadaye alichezea Nyota Nyekundu, Simba SC, Small Simba ya Zanzibar, Volcano ya Kenya alipokwenda na Zamoyoni Mogella na LiIa Shomari (pia marehemu) na Ndovu ya Arusha.
Alikuwemo kwenye kikosi cha Simba kilichokwenda ziara ya mafunzo nchini Brazil mwaka 1981.
Kisaka atakumbukwa kwa upole wake na ufanyaji kazi kwa bidii enzi za uhai wake. Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.

Source : BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment