Thursday, February 20, 2014

MIMI NI MTANZANIA NA NITABAKIA KUWA MTANZANIA

Baada ya Watanzania wa Ughaibuni na Watanzania wengine walioko Tanzania kuwakilisha maombi yao ya uraia wa nchi zaidi ya moja Serikalini na kwenye Bunge Maalumu la Katiba kumekuwa na Watanzania wengine waliodiriki kusema kuwa Watanzania wa ughaibuni ni wasaliti na hawahitaji kuwa Watanzania kwa sababu wameondoka nchini. 

Sisi Watanzania tunaoishi ughaibuni tunatofautiana na kauli hii na hapa tutaonyesha kwa nini kila Mtanzania huku Ughaibuni anasema “Mimi ni Mtanzania.”
Watanzania wengi bado wanaamini Tanzania ni nyumbani kwao. Bado wana mapenzi na Tanzania. Bado wana ndugu Tanzania na bado wanamiliki mali Tanzania. 

Baadhi yao bado wanalipa kodi zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi kutokana na umilikaji wao wa mali, ardhi na nyumba. Watanzania wa Ughaibuni bado wanafanya kazi kwa nguvu zote na sehemu ya mapato yao inaishia Tanzania.

 Watanzania hawa wanaamini kuwa wako ughaibuni kuboresha maisha yao kama ilivyo kwa raia wa nchi nyingine ambao uhama nchi zao na kwenda kuishi kwenye nchi nyingine. Kwa kifupi Watanzania wa ughaibuni sio tu waliohama nchi yao peke yao na hata huko waliko hukutana na raia wa mataifa mengine waliohama nchi zao.  

Sababu kubwa ya Watanzania wa Ughaibuni kuomba haki ya kubakia raia wa Tanzania ni kutokupoteza haki yao ya kuzaliwa Tanzania na kuwa karibu na ndugu zao pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa lao. Pia bado wana uzalendo na mapenzi na Tanzania.
Kwa nini Watanzania wa Ughaibuni wanaliomba Bunge Maalumu la Katiba liingize haki ya uraia wa nchi mbili kwenye katiba mpya?
Sehemu ya 59 ya rasimu ya pili ya Katiba ukurasa wa 23 inasema “… mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine, atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano, atakuwa na hadhi kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.” 

Watanzania tunaoishi ughaibuni ambao bado tuna mapenzi na Tanzania tunapochukua uraia wa pili tunapoteza uraia wa Tanzania ingawa sisi hatupendi kuupoteza. Hivyo, kwa mapenzi tuliyonayo kwa Tanzania, sisi Watanzania tunaoishi ughaibuni tunaliomba Bunge Maalumu la Katiba kurekebisha kIpengele hiki ili kiweke wazi kuwa Mtanzania hapotezi Utanzania wake kwa kupewa uraia wa nchi nyingine. 

Wengi wetu bado tuna mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania. Na bado tunajisikia Watanzania na tuna ndugu Tanzania, ndugu ambao bado tunawapenda kwa moyo wote na ambao hatutaki kutenganishwa nao.
Kwa mfano, Waafrika wa Kusini kutoka Afrika ya Kusini kwa mujibu wa Katiba yao ya mwaka 1996 hawapotezi uraia wao. Katiba ya Afrika Kusini imeweka wazi katika sura ya pili inayohusu haki za binadamu kuwa hakuna raia atakayenyang’anywa uraia wake.
Mfano mwingine mzuri ni kutoka Kenya. Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, sura ya tatu sehemu ya 16 inasema raia wa Kenya wa kuzaliwa hapotezi uraia wake kwa sababu ya kupatiwa uraia wa nchi nyingine.  
Katiba hizi mbili za Afrika  ya Kusini na Kenya zinatosha kabisa kutoa mwanga wa ni jinsi gani baadhi ya nchi za Kiafrika zinavyothamini raia wake. Nchi  hizi hazikubali kupoteza raia wake, kwa nini Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakubali kupoteza raia wake?
Kumekuwepo na malalamiko ya kwa nini  nyie mliojiripua mnataka kuwa Watanzania tena? Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya Watanzania wanaoishi nchi za nje hawakujiripua bali walikwenda mashule na vyuo mbalimbali Ughaibuni na wakati wengine walikwenda kwa shughuli za kikazi na kifamilia. Hivyo madai ya kuwa wote wamejiripua sio ya ukweli na hayana msingi wowote. 

Na tunaiomba Serikali, Bunge Maalumu la Katiba na Vyama Vyote vya Kisiasa kuyapuuza madai haya yasiyo na msingi wowote kwani hayahusiani na Watanzania wote waishio Ughaibuni. 

Sisi Watanzania wa Marekani, tunaiomba Serikali, Bunge Maalumu la Katiba na Vyama vya Siasa kulipigia kura suala la uraia wa nchi mbili ili kuhakikisha linapitishwa na Bunge Maalumu la Katiba na linawekwa kwenye Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi Watanzania wa Ughaibuni tunapenda kuwahakikishia Watanzania wote tuko tayari kushirikiana na Watanzania wote kulijenga taifa letu na kuleta maendeleo endelevu ambayo yanafaida kubwa kwa kila Mtanzania.
Imeandaliwa na Deogratius Mhella, Katibu wa Vikao vya Jumuiya za Watanzania Marekani na DICOTA katika jitihada za Watanzania waishio ughaibuni kuelimisha umma kuhusu Watanzania wa ughaibuni na kuhusiana na suala zima la uraia pacha.

No comments:

Post a Comment