KIPA Ivo Mapunda ametangaza rasmi kwamba anaondoka Simba na amemtaka kocha wake, Patrick Phiri, asimpange tena katika mechi zilizobaki za Ligi Kuu Bara kwani amechoka kutuhumiwa kuwa anaihujumu timu.
Ivo ametoa kauli hiyo baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Simba ilifungwa bao 1-0 yeye akiwa langoni. Mashabiki wamemlalamikia kuwa alifungwa bao hilo kizembe.
Ivo aliliambia Mwanaspoti kuwa hataki tena kukaa langoni katika mechi za Simba za ligi na nyinginezo kwani imani ya mashabiki kwake imepotea kwani hata akifungwa katika mazingira ya kawaida haeleweki.
“Nafanya kazi katika mazingira magumu mno, sina raha wala amani ndani ya timu, kila mechi nikidaka lazima nilaumiwe sasa kuna haja gani ya kuendelea kusimama langoni? Nitazungumza na kocha asinipange tena kudaka mechi zilizobaki, nataka nikae benchi,” alisema Ivo.
Hii ina maana Simba itapaswa kumtumia kipa chipukizi Manyika Peter katika mechi dhidi ya Mgambo JKT Jumapili wiki hii jijini Tanga.
source : mwanaspoti
No comments:
Post a Comment