Tuesday, March 24, 2015

MO Dewji Foundation yatoa msaada wa Baiskeli

DSC_0370
Mtendaji Mkuu wa MO DEWJI FOUNDATION, Gerald Mgesi David akimkabidhi rasmi kijana Paulo Ezekiel (23) msaada wa baiskeli ya magurudumu matatu (tricycle) itakayomsaidia katika kutembelea kwenye shughuli zake za kila siku.

Taasisi ya MO DEWJI FOUNDATION inayojishughulisha na miradi ya kusaidia jamii Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo Afya, elimu na maji mwishoni mwa wiki imeweza kumpatia kijana Paulo Ezekiel (23) msaada wa baiskeli ya magurudumu matatu (tricycle) itakayomsaidia katika kutembelea kwenye shughuli zake za kila siku.
Tukio hilo la makabidhiano limefanyika katika ofisi za Mo Dewji Foundation jijini Dar es Salaam ambapo Mtendaji Mkuu wa MO DEWJI FOUNDATION, Gerald Mgesi David alikabidhi msaada huo kwa kijana Paulo Ezekieli
Akizungumza na Modewjiblog, Mtendaji mkuu wa Mo Dewji Foundation amesema, waliguswa na usumbufu aliokuwa anaupata kijana na hivyo kuona ni vyema kumsaidia ili aweze kumudu kuendesha shughuli zake za kila siku.
Mo Dewji Foundation imejikita katika kutekeleza miradi ya kijamii ambayo inalenga kusaidia jamii ya kitanzania katika kujikwamua katika hali ya umaskini na kuinua kipato.
DSC_0399
Kijana Paulo Ezekiel (kulia) akiwa kwenye mahojiano na mwandishi wa habari wa modewjiblog, Andrew Chale.

Kijana Paulo Ezekiel:
Kwa upande wake, kijana Paulo Ezekiel ambaye muda mfupi baada ya kukabidhiwa baiskeli hiyo, alifanya mahojiano maalum na mtandao huu ambapo alieza kuwa, tatizohilo la kulemaa mguu, lilimtokea ghafla wakati yupo mitaa ya Kariakoo kwenye shughuli zake binafsi.
“Nakumbuka nilikuwa kwenye matembezi maeneo ya Kariakoo, ghafla nilipata kuhisi hali ya kupooza mguu mmoja wa kulia na kupoteza nguvu wasamaria wema waliniokota na kunipeleka Muhimbili” anaeleza Paulo Ezekiel.
Alieleza kuwa, alikaa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa muda wa miezi sita huku akipatiwa matibabu na baadae aliruhusiwa.
“Niliporuhusiwa hali ilikuwa ngumu sana. Kwani nilianza kuomba omba kwa watu msaada ikiwemo kifaa cha kuniwezesha kunisaidia kutembelea. Kule Muhimbili nilikuwa natumia baiskeli kutembelea hivyo nilivyoruhusiwa iliniwia vigumu sana kutumia vifaa vya ulemavu ikiwemo haya magongo.
Kuna siku katika kuomba omba. Nilikutana na mtu mmoja ambaye alinielekeza kwa Mh. Dewji. Nilipofika kwake msaidizi wake alinitaka nifuatilia kuona kama watafanikisha kwani tayari bajeti ilikuwa imeshafungwa hadi kipindi kingine” alieleza Paulo Ezekiel.
DSC_0373
Hata hivyo Paulo Ezekiel alibainisha kuwa, wakati yupo nyumbani kwao, alipigiwa simu juu ya kuitwa kukabidhiwa baiskeli hiyo.
“Sikuamini kama ningeweza kupata msaada huu. Hadi nilipofika hapa kukabidhiwa namshukuru Mungu pia namuombea kwa Mungu Mh. Mohammed Dewji kwa msaada wake, kwani simjui na wala hanijui..Ilikuwa ni kama bahati kufika katika ofisi yake na kuomba msaada huu asante sana na namuombea maisha marefu Dewji na familia yake, wafanyakazi wake wote popote pale kwani kuniwezesha mimi ni ubinadamu mkubwa sana” alimalizia kijana Paulo Ezekiel.
Paulo Ezekiel anabainisha kuwa, ilikua vigumu sana kwa yeye kutembelea magongo siku za mwanzoni ambapo anasema hakuwahi kutegemea kama siku moja atakuja kuwa mlemavu.
“Hujafa, hujaumbika naamini hilo, kwani awali nilikuwa najitafutia riziki zangu za kujikimu kimaisha lakini nilipopata tatizo hili la kupooza mguu na kulemaa ndoto zangu zote zimeyeyuka ila sijakata tama” Hivi ndivyo anavyomalizia Paulo Ezekiel ambaye anaishi Mbagala, Temeke Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
DSC_0397
Mwandishi wa habari wa modewjiblog, Andrew Chale (kushoto) akifanya mahojiano na Paulo Ezekiel mara baada ya kukabidhi msaada wa baiskeli ya magudumu matatu.
Kijana huyu awali alikua akifanya shughuli za kutafsiri Lugha kwa wageni wanaokuja kununua bidhaa kwenye maduka ya Kariakoo na Bandari ya Dar es Salaam hasa wafanyabiashara wanaotoka Congo, Rwanda, Zambia, Malawi, Burundi na maeneo mbalimbali.
Paulo Ezekiel ni mtoto wa pili kati ya watoto nne, anatokea Mkoa wa Kilimanjaro na kabila lake ni Mchaga.
DSC_0317-1024x682
MO DEWJI FOUNDATION: Ni taasisi iliyoanzishwa na Mbunge wa Singida Mjini (CCM) na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarufu ‘MO’ (pichani) ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya kiongozi bora aliyejitolea kwa kiasi kikubwa katika jamii na kuleta mabadiliko Afrika kwa mwaka 2014.
Tuzo hiyo aliyotunukiwa MO iitwayo African Philanthropist of the year Award 2014, Ilitolewa na jarida la uongozi la Uingereza, jijini Dubai wakati wa Jukwaa la Viongozi wa Afrika.
Kabla ya kukabidhiwa tuzo hiyo, sifa kuu aliyokuwa nayo MO kama alivyofafanua wakati wa kukabidhiwa tuzo hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa jarida hilo, Dk Ken Giami alisema wataalamu waelekezi walimchagua Dewji kuwa mshindi kutokana na: Uongozi bora katika Kampuni yake ya Mohammed Enterprises (MeTL GROUP) Pia kigezo kingine kilichompa ushindi ni namna anavyojihusisha na kazi mbalimbali za kijamii.
Pia Mchango wa MO katika elimu ni sehemu kubwa ya mafanikio yake hususan kwa kuendeleza ujenzi wa shule mbili hadi 12, pamoja na kujitolea kiasi cha zaidi ya Sh520 milioni katika kuendeleza sekta hiyo ya elimu ndani ya jimbo lake hilo la Ubunge la Singida Mjini.
MO pia amekuwa akisaidia sekta ya afya kwa ushirikiano na Taasisi ya Bilal Muslim Mission ya Tanzania kwa kuwaleta madaktari waliowafanyia upasuaji wagonjwa wa macho na 179 kupata miwani, kusambaza maji safi na salama kwa kuchimba visima vingi vya maji ndani ya jimbo na n.k.
Kwa sasa MO ndie Bilionea kijana Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes. Unaweza kusoma zaidi kupitia http://www.forbes.com/profile/mohammed-dewji/
Kwa hali hiyo pia Dewji ameingia katika orodha ya Philanthropist duniani pia waweza kuona watu wengine waliotunukiwa tuzo kama hiyo kupitia hapa: http://en.wikipedia.org/wiki/List_of_philanthropists
Msomaji wetu unaendelea kuperuzi mtandao wako wa Modewji blog, tutakuletea makala maalum juu ya tatizo hili la kupooza ghafla kwa viungo hadi kusababishia kilema. Endelea kuwa nasi. Asante pia waweza kutuma maoni yako kupitia hapo chini ndani ya mtandao huu ama kupitia simu 0719076376 au 0689858799 au email info@modewjiblog.com

No comments:

Post a Comment