Thursday, February 11, 2021

TUNAMFICHA NANI? KWA NINI? NA KWA FAIDA GANI?

 

Rev. Godwin Chilewa akiwa amelazwa katika moja ya hospitali jijini 
Houston, Texas akiugulia Covid-19

Rev. Godwin Chilewa akiwa Zanzibar na mkewe

Na Rev. Godwin Chilewa
Nimeugua Covid 19, nikatibiwa na kupona (Jina la Bwana lihimidiwe). Kuugua kwangu kumenisaidia kujifunza mengi, na kubaini uongo mwingi wanaoambiwa watu wetu ili kuwapooza, badala ya kufanya jitihada ya dhati ya kuwalinda, na kuwaokoa na janga la Covid 19. Ni kwa sanabu hii nimeona vema kuandika machache kuhusu ugonjwa huu.

Nianze kwa kuweka bayana kuwa naishi nchini Marekani, lakini niliambukizwa Covid-19 nchini Tanzania nilikokuwa nimeipeleka familia yangu kusherehekea siku kuu ya christmas na mwaka mpya.

Tuliwasili Tanzania tarehe 6 Desemba 2020 tukitokea Houston. Siku mbili kabla ya kuondoka Marekani, mimi na familia yangu tulipimwa na kuthibitishwa hatukuwa na virusi vya Covid-19 kigezo muhimu cha kuturuhusu kutoka nje ya nchi. Baada ya kuwasili Tanzania tulikaa Dar es Salaam, tukazungukia vivutio vya utalii vya Serengeti na kumalizia likizo yetu Zanzibar.

Siku mbili kabla ya kuondoka Tanzania tulikwenda hospitali ya Muhimbili kupima covid-19 ili tuweze kupata cheti cha kuturuhusu kutoka nchini kwa mujibu wa taratibu na maagizo ya wizara ya afya. Mimi na familia yangu (mke na watoto watatu) tulilipa dola mia tano ($500) gharama za vipimo hivyo. Tarehe 14 January tulipokea majibu na vyeti kuwa sote tulikuwa ‘Negative’ na kesho yake tarehe 15 January 2021 tuliondoka kwa ndege kurudi Marekani. Cha ajabu ni kuwa nilianza kuumwa nikiwa kwenye ndege.

HALI YA TANZANIA
Ukiwasikiliza viongozi wetu wanapozungumzia ugonjwa wa covid-19 utasikia wakisisitiza suala moja tu “Piga nyungu” na tumia kinywaji cha tangawizi, limao na vitunguu swaumu kuongeza kinga ya mwili wako. Maneno haya yaliyoanzia kwa wanasiasa, na kubebwa na wataalam wa afya yamesambaa kama moto katika nyasi kavu na kisha kuzama katika mioyo ya watu wengi wenye imani na viongozi wao.
Ukitafakari kwa kina utagundua kuwa kampeni hii ya kuvutia imewafanya watanzania kuitua mzigo serikali kwa kuamini wanaweza kujitibu wenyewe, hawapaswi kuisumbua wala kuihoji serikali kuhusu HATUA za dhati inazochukua katika kupambana na maambukizi mapya, kufungua vituo vipya vya tiba ya Covid-19, Kuboresha matibabu ya Covid 19, na au kushughulikia suala la chanjo

Swali la kujiuliza ni je! Nyungu inatibu? Na je! ni kweli kuwa kinywaji cha tangawizi, limao na vitunguu swaumu vinaweza kukuponya endapo utapata maambukizi makali ya covid 19 ?

UGONJWA COVID-19.
Siku mbili baada ya kuwasili Marekani, hali yangu ilikuwa mbaya sana; mwili na mifupa yote ilikuwa ikiniuma vibaya sana, kichwa kilikuwa kikigonga kana kwamba kinataka kupasuka, na joto la mwili wangu lilikuwa juu mno kiasi cha nyuzi joto 103 F na lilikuwa haliteremki. Nilipelekwa katika kituo cha kupimia virusi hivyo na kubainika kuwa ni POSITIVE. Mara moja familia yangu, jamaa na marafiki toka Tanzania wakanishauri kupiga nyungu na kutumia tangawizi, vitunguu swaumu na vidonge vya vitamin lukuki vinavyopatikana hapa. Nilifanya hivyo kwa siku mbili mfululizo, huku nikiendelea kutumia vidonge vya kushusha homa bila mafanikio.

Siku ya tatu hali ilikuwa mbaya sana. Licha ya homa kutoteremka kabisa, nilianza kushindwa kupumua, na blood pressure yangu ilikuwa imepanda kuliko kawaida. Mke wangu akanikimbiza Methodist Hospital, mojawapo ya hospitali kubwa zinazoheshimika nchini Marekani. Nikapokelewa na kulazwa, nikawekewa Oxygen na kupewa dawa za kushusha homa, kisha kazi ya uchunguzi wa kitabibu ikaanza.

Kwanza manesi walichukua sampuli zaidi ya kumi za damu na kuzipeleka maabara. Muda mfupi baadae nilifanyiwa X-ray ya mapafu, na baadae nikafanyiwa CT scan ya mapafu kuangalia undani wa maambukizi. Vipimo vyote vilikuwa tayari baada ya saa moja hivi, na daktari akaja kunipa maelezo ya hali yangu:

JINSI COVID-19 INAVYOUA

Labda nisisitize hapa kuwa virusi vya Corona humshambulia kila mtu kwa namna tofauti. Mashambulizi hayo huweza kuwa mabaya sana (severe) au madogo tu (mild) kutegemea hali ya ki afya ya mtu mwenyewe, uwezo wa mwili wake katika kupambana na maradhi, na aina ya vijidudu vilivyomshambulia. Hata hivyo kutokana na hali halisi ya watanzania, wengi wanaweza kuangukia katika kundi hatarishi.

Baada ya kupokea matokeo ya vipimo vyangu Daktari alianza kwa kunipooza kuwa “You’re in good hands, so don’t worry, you will be fine“ kisha akaendelea kunieleza ukweli mchungu ambao natamani kila mtu aufahamu na kuzingatia.

Alinieleza kuwa virusi vya covid-19 vilikuwa vimepenya katika mapafu na kunisababishia pneumonia. Hali hii ilikuwa inaendelea kuwa mbaya kwa kadri muda ulivyokuwa ukienda na ndiyo iliyokuwa ikinifanya nishindwe kupumua.

Virusi vya corona vinasababisha damu kuganda hivyo aliniambia upo uwezekano nikapata blood clots ndogondogo (miner) au mbaya (severe) kwenye ubongo, moyo au mapafu. Akafafanua kuwa endapo damu itaganda kwenye ubongo hawatakuwa na uwezo wa kufanya lolote “ there is nothing we can do” isipokuwa kama ni kwenye mapafu au moyo wanaweza kuishughulikia (We can do something).

Mapigo ya moyo wangu (BP) yalikuwa juu mno hali iliyoleta wasiwasi kuwa naweza kupata kiharusi. Mapigo hayo yalipandishwa mno na maumivu ya mwili, pamoja na homa kali iliyokuwa haiteremki. Ilibidi niwekwe kwenye uangalizi maalum.

Jambo lingine ni kuwa virusi vya corona huweza kukuletea KISUKARI cha muda. Hii ina maana hata kama wewe huumwi, wala hujawahi kuwa na historia ya ugonjwa wa kisukari, Covid-19 inaweza kupandisha sukari ya mwili wako kwa kiwango cha kukuua. Hali hiyo huongezeka zaidi endapo utapewa madawa aina ya steroids kukusaidia kupunguza athari ya covid (inflammation) katika mapafu.

Mapafu na mwili mzima kujaa maji ni tatizo lingine kubwa linaloweza kukuondoa duniani haraka. Virusi vya corona husababisha viungo vya mwili (body organs) kuhifadhi maji ya ziada. Kwa sababu zile siku mbili za mwanzo nilikunywa maji mengi ya tangawizi na limao, mwili wangu ulikuwa tayari umehifadhi maji mengi kuliko inavyotakiwa hali iliyoyapa mapafu ugumu wa kufanya kazi yake.

Daktari pia alinishangaa na kunionya vikali kuhusu suala la kupiga nyungu (kujifukiza) baada ya mimi kumuuliza kama hiyo ilikuwa “first aid sahihi” Aliniambia kuwa kitu nilichofanya kilikuwa kutaka kujiua mwenyewe (sucide) na alishangaa nimewezaje kunusurika. Alifafanua kuwa covid-19 hudhofisha mapafu, na kupunguza kiwango cha hewa ya Oxygen inayoingia katika mzunguko wa damu na kwenda kwenye ubongo. Zile dakika tatu au tano unazojifunika na kujifukiza mvuke hupunguza zaidi kiwango cha hewa safi inayoenda katika ubongo wako hali inayoweza kusababisha kuanguka ghafla na kufa. Alisisitiza mgonjwa wa Covid-19 anahitaji oxygen sio mvuke.

MATIBABU

Ili kukabiliana na hali niliyokuwanayo Daktari alinifanyia mpango wa matibabu ufuatao:

Aliagiza nipewe madawa ya kupambana na bakteria kwa ajili ya kuua wadudu walioingia kushambulia mapafu na kunipa pneumonia. Dawa hizi nilipewa kwa kuchomwa kwenye mishipa (drip).

Aliagiza nipewe plasma (damu ya mtu mwingine) aliyeugua ugonjwa wa corona na kupona. Plasma ya mtu hiyo kwa vile tayari ina antibodies zilizoweza kupambana na virusi vya corona na kuvishinda ilionekana itaweza kuusaidia mwili wangu kuimarisha mapambano na vijidudu hivyo.

Aliagiza nipewe dawa mpya ya kupambana na virusi vya corona iitwayo Remdesivir iliyoonesha ufanisi katika kupambana na ugonjwa huo. Mgonjwa hupewa dawa hii kupitia mishipa ya damu (drip).

Kushusha mapigo ya moyo na kuendelea kudhibiti hali hiyo nilipatiwa dawa za aina mbili tofauti (moja asubuhi na nyingine jioni) huku wauguzi wakifuatilia kwa karibu hali inavyoendelea.

Aliagiza nipewe dose ya steroids mara mbili kwa siku ili kusaidia kupunguza inflammations katika mapafu. Hili lilienda sambamba na madawa ya kushusha homa niliyopewa kila baada ya masaa manne.

Aliagiza nichomwe sindano za insuline ili kudhibiti sukari iliyokuwa ikipanda hovyo. Ingawa mimi sina historia ya kisukari, wala ukoo wetu hatuna historia ya kisukari, covid-19 ilinipa kisukari cha muda, na kama nisingeenda hospitali kutibiwa nisingejua kabisa. Nilichomwa sindano hizo kila siku kwa muda wa siku sita niliokuwa nimelazwa hospitali.

Aliagiza nichomwe dawa ya kuyeyusha damu (blood thinners) ili kuzuia uwezekano wa damu kuganda (blood clots) katika ubongo, moyo na mapafu. Sindano hizi nilichomwa tumboni, mara mbili kwa siku, kwa muda wa siku sita.

Kwa vile viungo vya mwili (body organs) zilikuwa zimejaa maji ya ziada, aliagiza nichomwe diuretic ili zinisukume kwenda haja ndogo mara nyingi kupunguza maji mwilini. Sindano hizi nilichomwa mara mbili kwa siku kwa siku sita.

Kutokana na wingi wa madawa niliyokuwa nikitumia daktari pia aliagiza nipewe vidonge maalum vya kuzuia tumbo lisiathirike na kutengeneza vidonda vya tumbo.

Pengine utajiuliza kwa nini nimechukua muda kuelezea mlolongo wa matibabu nilioupata katika nchi ya dunia ya kwanza, huku nikijua kuwa si rahisi kwa mtanzania wa kawaida kuyapata? Naomba nieleweke hapa kuwa lengo langu ni kuwafumbua macho walio wengi kuwa ugonjwa wa covid-19 si wa mzaha, madhara yake ni makubwa, na hautibiki ki rahisi kama viongozi wetu na wataalam wa afya wanavyodai, na kusisitiza kuwa kupiga nyungu, na kikombe cha tangawizi au chupa chache za dawa za asili zinaweza kumponya mgonjwa wa covid-19. Huu ni uongo mbaya unaoshambulia maeneo tofauti ya mwili, na kuweza kukupa magonjwa mengine ambayo hujawahi kuugua. Hebu fikiria madhara anayoweza kupata mtu kwa kunywa kikombe cha tangawizi yenye sukari pasipo kujua kuwa covid-19 imeshampa kisukari!

HADAA KWA WAGENI
Jambo lingine linalonikera ni hadaa ya kijinga inayofanywa kwa wageni na wasafiri. Mwanzoni mwa mwezi Januari 2021 serikali kupitia waziri wake wa fedha iliyoa agizo la kutaka watu wote (Pamoja na watalii) wanaotaka kutoka nchini kupimwa covid-19 (Kwa gharama ya USD 100) na kupewa cheti cha kuthibitisha usalama wao. Agizo hilo lililoonekana kama lenye umuhimu na lengo la kuzuia kusambaa kwa maambukizi mapya limeishia kuwa kitega uchumi ka Taifa. Wengi wa wageni wanaopimwa kama ilivyoelekezwa hawapewi majibu sahihi, na kwa wakati kama inavyotakiwa. Hii ni kwa sababu wapimaji wamepewa maelekezo kutoweka bayana kwamba Tanzania kuna Covid-19 na hivyo kulazimika kutoa majibu ya uongo.

Ukweli huu unaweza kuthibitishwa kwa kufuatilia idadi ya wasafiri toka Tanzania wanaougua covid-19 mara tu baada ya kuwasili katika nchi wanazokwenda (Final destinations). Nikiwa hospitali ya Muhimbili nilikutana na wageni kadhaa waliokuwa wakilalamikia kupigwa danadana kwa majibu yao. Pamoja na hilo mimi mwenyewe pia nilipimwa na kupewa majibu ya uongo kuwa ni sina vijidudu vya corona (Negative) wakati kumbe nilikuwa na virusi hivyo. Namshukuru Mungu kuwa uongo wao uliniwezesha kurudi Marekani, na kupata tiba stahiki. Hata hivyo nasikitika kwani sijui uongo huo ulisababisha kuwaambukiza watu wangapi ukizingatia kuwa nilianza kuumwa nikiwa kwenye ndege.

HADAA YA TIBA ASILIA
Kama nilivyoeleza hapo juu, hivi sasa viongozi na wataalam wetu wa afya wamejikita katika kuhimiza upigaji nyungu, na matumizi ya dawa asilia. Lakini je! hizi dawa zinatibu kweli au ni placebo tu? Bila shaka mtu yeyote mwenye akili timamu atatambua kuwa kinachoendelea ni utaratibu wa kuwatoa hofu watanzania, kwa placebo na maneno ya faraja. Lakini je, nchi inafanya nini kumuokoa mtanzania?

Hebu tikiulize, kwanini serikali haiweki bayana mipango yake ya muda mrefu na muda mfupi katika kupambana na ugonjwa huu? Kwa nini waziri wa afya asisimame kuwaambia watanzania kuwa imefunguliwa center kubwa ya kuhudumia wagonjwa wa corona, na wote wanaougua ugonjwa huo watapelekwa huko kupatiwa matibabu stahiki?? Kwa nini serikali haisemi tangu ugonjwa huu ulipoanza imeingiza nchini mashine ngapi za kuwasaidia wagonjwa mahututi kupumua? Kwanini haisemi imetumia kiasi gani kuagiza madawa ya kisasa kama Remdesivir na mengineyo? Kwa nini hata haizungumzii au ku promote matumizi rahisi ya plasma katika kutibu ugonjwa huo?? Kulikoni?

HITIMISHO
Ni dhahiri kuwa kuna tatizo kubwa katika kushughulikia ugonjwa huu kuliko wengi tunavyojua. Ni vema watanzania wote tukatafakari upya na kuwahoji viongozi wetu ili walieleze taifa ukweli. Waseme ni kitu gani kinachowazuia kwenda sambamba na jumuia ya kimataifa, pamoja na mashirika kama WHO katika kupambana na ugonjwa huu. Ni hatua gani wanachukua katika kuboresha matibabu ya covid 19 katika hospitali zetu, na kwa kutumia taaluma ya kisasa badala ya mitishamba.

Mimi binafsi ningependa kujua kama serikali kupitia wizara ya afya imewahi kuagiza na kusimamia matumizi ya plasma na dawa aina ya Remdesivir kwa wagonjwa wa corona nchini. Mpaka sasa muungano huo umeonesha uwezo wa kuwasaidia wagonjwa wa covid-19 ikiwa pamoja na mimi mwenyewe..

Hili ni jukumu letu sote.
Uwe na amani

No comments:

Post a Comment