Friday, July 20, 2012

YANGA YAWACHAPA APR 2-0


OGOPA JEZI NAMBA 11 YANGA; Said Bahanuzi akishangilia kwa
 staili ya kuonyesha jezi namba yake baada ya kufunga bao leo

Na Prince Akbar
YANGA imeonyesha matumaini ya kutetea taji lake la Klabu Bingwa Afrika 
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kuifunga APR ya Rwanda 
mabao 2-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.

Shujaa wa Yanga leo, alikuwa ni mshambuliaji mpya kutoka Mtibwa Sugar ya 
Morogoro, Said Bahanuzi, aliyefunga mabao yote hayo, moja kila kipindi.
Hadi mapumziko, tayari Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Bahanuzi 
dakika ya 22, akiunganisha krosi ya Hamisi Kiiza.
Dakika ya 43, Bahanuzi alitupia tena mpira nyavuni, pasi ya Kiiza, lakini refa 
Dennis Batte kutoka Uganda akakataa.
Kipindi cha pili, Yanga waliendelea kucheza kwa kuelewana na kasi, 
wakilitia misukosuko muda wote lango la APR na dakika ya 67, beki mmoja 
wa APR alikuwa anataka kumpiga chenga Bahanuzi kwenye eneo la hatari, 
lakini mshambuliaji huyo akafanikiwa kuunasa mpira huo na kumtoka beki huyo 
kabla ya kumchambua kipa Jean Claude Ndoli.
Lilikuwa bao tamu, ambalo liliwanua vitini mashabiki wa Yanga na kuamini sasa 
wameshinda mechi.
Kocha Tom Saintfiet alimpumzisha Bahanuzi dakika ya 72 na nafasi yake
ikachukuliwa na Jerry Tegete, wakati Nizar Khalfan kabla ya hapo alimpisha 
Juma Seif ‘Kijiko’.

Kwa ushindi huo, Yanga imemaliza mechi za Kundi C ikiwa katika nafasi ya pili 
kwa pointi zake sita, mabao tisa ya kufunga, matatu ya kufungwa, Bahanuzi 
akiwa amefunga manne kati ya hayo, akifuatiwa na Hamisi Kiiza mwenye matatu, 
moja Stefano Mwasyika na lingine Nizar Khalfan.
Atletico ya Burundi inaendelea kuongoza Kundi C, kwa pointi zake saba, baada 
ya kucheza mechi tatu, kushinda mbili na kutoa sare moja, wakati APR ya 
Rwanda inashika nafasi ya tatau nayo imefuzu Robo Fainali, kwa pointi zake 
nne, wakati Waw Salaam ambayo haina pointi na imeaga.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma Abdul, 
Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, 
Stefano Mwasyika, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi/Jerry Tegete, Hamisi Kiiza 
na Nizar Khalfan/Juma Seif.

A.P.R.;  Jean Claude Ndoli, Mbuyu Twite, Kabange Twite, Mugiraneza Jean, 
Leonel St Preus, Johnson Bagoole, Iranzi Jean Claude, Ngabo Albert, Tuyizere 
Donatien, Suleiman Ndikumana na Olivier Karekezi.
Nahodha Cannavaro akimpongeza kijana

Kiiza akiwa amembeba juu Bahanuzi 

Bahanuzi anakwenda kufunga la pili

                   Kiiza alikosa bao la wazi hapa

Daktari wa Yanga, Sufiani Juma akimtibu Bahanuzi 
                         Kona langoni mwa APR

No comments:

Post a Comment