Friday, September 28, 2012

Manji amwaga mil.100 Kuiua Simba Oktoba 3

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji
KIKOSI cha timu ya Yanga kimeingia kambini jana katika Hotel ya Uplands iliyopo Changanyikeni jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi yake dhidi ya mahasimu wao Simba itakayopigwa Oktoba 3, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo jana zinaeleza uongozi umefikia hatua ya kuweka kambi kutokana na utulivu iliopo eneo hilo wakiamini wachezaji watapata wasaa mzuri wa kujiandaa na mechi hiyo itakayochezwa Jumatano.
Kabla ya kucheza na Simba, Yanga inayojifua kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, keshokutwa itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kucheza na African Lyon.
Yanga yenye pointi nne ilizovuna kwenye mechi tatu ilizocheza tangu kwanza kwa ligi hiyo Septemba 15, Jumapili hii itakuwa ikipigania ushindi kwa Lyon kujiweka fiti kisaikolojia pia kufikisha pointi saba kabla ya kucheza na Simba.
Aidha, Yanga chini ya Kaimu Kocha Mkuu wake Fred Felix Minziro, itawakabili Simba wakikumbuka kisago cha mabao 5-0, walichopata katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya msimu uliopita ambayo ilihitimishwa Mei 6.
Kwa kutambua umuhimu wa pointi tatu katika mechi hiyo ya watani wa jadi, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji aliyeingia madarakani Julai 15, ametoa sh milioni 100, kuamsha hamasa ya maandalizi kwa wanachama kuelekea mechi hiyo.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya klabu hiyo kimedokeza kuwa, Manji ametoa fedha hizo kuamsha hamasa kwa ajili ya kuisapoti timu yao wakati wote wa mechi na kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili kupata ponti tatu na kurejesha heshima ya klabu hiyo.
 
Yanga iliyoanza ligi hiyo kwa sare ya bila kufungana na Prisons kabla ya kufungwa 3-0 na Mtibwa Sugar, ilizindukia kwa JKT Ruvu kwa kuinyuka 4-1, huku Simba ikiwa na rekodi ya kushinda asilimi 10, ikishinda mechi zote tatu.
Wakati Yanga itakutana na Simba ikitoka kucheza na Lyon, mabingwa watetezi Simba ambao wamejichimbia visiwani Zanzibar, watakutana na wakali hao wa Jangwani wakitokea kucheza na Tanzania Prisons ya Mbeya, mechi itakayochezwa kesho Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
 
Aidha, wakati Simba chini ya kocha wake Mserbia, Milovan Cirkovic siku hiyo itaikabili Yanga bila nyota wake wa kimataifa Mganda, Emmanuel Okwi, Yanga wao watakuwa bila Kocha Mkuu wake, Mbelgiji Tom Saintfiet, aliyetimuliwa.

No comments:

Post a Comment