*Ni kutokana na kushindwa kuwaengua Chenge, Lowassa
*Atamba Chadema kushinda uchaguzi wa jiji Mwanza leo
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Dk.Wilbrod Slaa, amesema kuwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kimeonyesha kila dalili ya kufa baada ya kushindwa
kuwaengua katika nafasi za kuwania uongozi watuhumiwa wakubwa wa
ufisadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana katika mahojiano maalum yaliyofanyika kwenye Hoteli ya Midland, Dk. Slaa alisema alitarajia kuwa CCM kingetumia fursa hiyo kujisafisha dhidi ya ufisadi kwa kuwaengua mapema wale wote waliokumbwa na kashifa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana katika mahojiano maalum yaliyofanyika kwenye Hoteli ya Midland, Dk. Slaa alisema alitarajia kuwa CCM kingetumia fursa hiyo kujisafisha dhidi ya ufisadi kwa kuwaengua mapema wale wote waliokumbwa na kashifa hizo.
“Katika hili nisingependa kumumunya maneno,
sioni dhamira ya CCM kujirekebisha hasa kwa vile imeshindwa kuwaengua
watuhumiwa wakubwa wa ufisadi,” alisema.
Alidai kwamba Mbunge wa
Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ambaye amepitishwa kuwania Ujumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia Wilaya ya Bariadi, mkoani
Simiyu, ni mtuhumiwa ambaye ushahidi upo wazi kuwa alikula rushwa
kupitia ununuzi wa rada, lakini chama hicho bado kimemuona anafaa kuwa
kiongozi.
“Mtu kama Chenge eti naye amepitishwa. Wote tunafahamu
kwamba alikutwa na pesa nyingi sana kwenye akaunti yake ya nje na
alipoulizwa akadai eti ni za urithi, alipobanwa zaidi akadai eti
alizipata baada ya kutoa ushauri, akaulizwa aliwezaje kufanya kazi hiyo
wakati alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akakosa jibu,” alisema Dk.
Slaa.
Aliongeza kwamba binafsi (Dk. Slaa) alipeleka ushahidi kwa
Mkurugnzi wa Mashitaka (DPP) kuhusu tuhuma hizo za ufisadi dhidi ya
Chenge, lakini CCM wamemuona kuwa ni kiongozi anayefaa kukiongoza chama
hicho.
Katibu Mkuu huyo wa Chadema pia alimgusia Waziri Mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kwamba ni miongoni mwa watuhumiwa wakubwa
wa ufisadi, lakini CCM kimempitisha kuwania ujumbe wa NEC kupitia
Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.
“Kabla sijaondoka bungeni
nilimwambia Lowassa kwamba kwa vile amejiuzulu kwa madai kwamba
anawajibika, ina maana alikuwa anamjua mtu aliyesababisha ajiuzulu,
hivyo tukamtaka amtaje ili sisi tumsafishe, lakini akashindwa kumtaja,”
alisema.
Chenge alituhumiwa kukutwa na Dola za Marekani milioni moja katika akaunti yake kwenye kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.
Fedha
hizo zilihusishwa na fedha za ununuzi wa rada ya kijeshi ambayo
Tanzania iliuziwa na Kampuni ya BAE-Systems ya Uingereza mapema miaka ya
2000 kwa bei ya juu tofauti na bei halisi.
Hata hivyo, mara kwa mara Chenge amekuwa akikanusha kuhusika na kashfa hiyo.
Hivi
karibuni, Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Wahariri wa vyombo vya
habari Ikulu, jijini Dar es Salaam, alimsafisha Chenge kwa kusema kuwa
hapakuwepo na rushwa katika ununuzi wa rada.
Kwa upande wake,
Lowassa ambaye alijiuzulu mapema Februari 2008, anatuhumiwa kuhusika
katika mchakato wa kutoa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa
Kampuni ya Richmond ya Marekani kwa njia za upendeleo.
Kampuni
hiyo ilipewa zabuni ya kuzaliwa megawati 100 wakati wa ukame mwaka 2006,
lakini baadaye ilidaiwa kutokuwa na uwezo wa kuzalisha umeme huo na
kulilazimisha Bunge kuunda Kamati Teule ya Uchunguzi chini ya uenyenkiti
Mbunge wa Kyela, Dk. Harisson Mwakyembe.
Kamati hiyo iliwasilisha taarifa yake bungeni na kusema kuwa Richmond ilikuwa kampuni hewa, hivyo kumshauri Lowassa atafakari.
Mwingine aliyejiuzulu kutokana na sakata la Richmond ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.
Hata hivyo, Karamagi naye amepitishwa na CCM kugombea ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Bukoba Vijijini, mkoani Kagera.
ASEMA CHADEMA KITASHINDA UMEYA
Katika
hatua nyingine, Dk. Slaa ambaye amekuwepo jijini Mwanza kusimamia
uteuzi wa wagombea nafasi za mameya na manaibu wao katika uchaguzi
utakaofanyika leo kwenye Halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya
Ilemela, alisema chama chake kitashinda katika uchaguzi huo.
Alisema
licha ya migogoro ambayo iliibuka ndani ya Chadema iliyosababisha
madiwani kumung’ao aliyekuwa Meya kupitia chama hicho, Josephat
Manyerere, kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye, lakini chama
hicho bado kiko imara.
Aidha, alisema hata baada ya Chadema
kuwafukuza uanachama madiwani wake wawili, Henry Matata wa Kata ya
Kitangiri na Adam Chagulani wa Kata ya Igoma, lakini wananchi wasiwe na
wasiwasi kwa sababu wamejipanga vizuri kuhakikisha chama hicho
kinaongoza Halmashauri zote mbili.
Alifafanua kwamba Chadema
hakina mgogoro isipokuwa hali hiyo imetokana na watu wengi, wakiwemo
baadhi ya madiwani kutofahamu vizuri katiba ya chama hicho.
Alibainisha
kwamba kinachodaiwa kuwa mgogoro ndani ya Chadema hasa katika Wilaya ya
Ilemela kimefafanuliwa vizuri sana katika kanuni na maazimio mbalimbali
ya vikao vya chama hicho, lakini wapo baadhi ya watu ambao wanapotosha
kwa makusudi.
Katika uchaguzi wa mameya wa Halmashauri za Jiji
la Mwanza na Manispaa ya Ilemela unaotarajia kufanyika leo, kuna mchuano
mkali kati ya Chadema na CCM huku kila chama kikichanga karata
kuhakikisha kinanyakua nyadhifa hizo.
Kwa upande wa Manispaa ya
Ilemela ambayo imemegwa kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Chadema
kina Madiwani wanane na Mbunge mmoja, hivyo kuwa na jumla ya kura tisa
wakati CCM kina Madiwani watano na Mbunge mmoja hivyo kuwa na jumla ya
kura sita.
Hata hivyo kuna uwezekano wa Chadema kubakiwa na kura
nane baada ya kumfukuza uanachama Diwani wa Kitangiri, Henry Matata,
ambaye hata hivyo, kuna taarifa kuwa atashiriki uchaguzi huo kwa sababu
ana pingamizi la mahakama kupinga hatua hiyo ya kufukuzwa, ingawa
Chadema pia kimesema hakitambui pingamizi hilo.
Pia katika
Halmashauri hiyo ya Ilemela, kuna Mbunge mmoja wa CUF ambaye kuna kila
dalili kwamba atashirikiana na Chadema katika uchaguzi huo.
Kwa
upande wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Chadema kina Madiwani saba na
Mbunge mmoja hivyo kuwa na jumla ya kura nane, lakini kinaweza kuwa na
kura mbili za ziada kutoka kwa Madiwani wawili wa CUF baada ya
kukubaliana kuwaachia nafasi ya Naibu Meya.
Hata hivyo, huenda
Chadema kikakosa kura ya Diwani wa Igoma, Adam Chagulani, ambaye
alifukuzwa uanachama, lakini kama atashiriki uchaguzi huo kwa amri ya
mahakama kama ilivyo kwa Diwani wa Kitangiri na akaamua kumpigia kura
mgombea wa CCM kutasababisha mchuano kuwa mkali.
Hali hiyo
inatokana na ukweli kwamba katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, CCM
kina madiwani saba, lakini kuna tetesi ambazo Chadema kinazilalamikia
kwamba kuna mchezo unaofanyika kumhamisha Mbunge Maria Hewa (CCM) kutoka
Manispaa ya Ilemela ili apige kura kumchagua Meya wa Jiji.
No comments:
Post a Comment