Tuesday, September 11, 2012

SIMBA SC YATWAA NGAO

Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga (kulia) akimkabidhi Ngao ya Jamii, Nahodha wa Simba, Juma Kaseja. Pembeni yake ni beki Nassor Masoud 'Chollo' na kulia kabisa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani. 
SIMBA SC, inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager imetwaa Ngao ya Jamii, baada ya kuifunga Azam FC, mabao 3-2 jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar e s Salaam.
Shujaa wa Simba leo hii alikuwa ni kiungo Mwinyi Kazimoto aliyefunga bao la ushindi dakika ya 78 kwa shuti kali la mbali baada ya kumchungulia kipa wa Azam, Deo Munishi ‘Dida’ amekaaje.
Hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na John Raphael Bocco ‘Adebayor’ na kipre Herman Tchetche, wakimtungua kipa namba moja Tanzania, Juma Kaseja.
Bocco alitangulia kufunga dakika ya tano ya mchezo huo, baada ya kupigiwa kona fupi na Abdi Kassim ‘Babbi’, akatoa pasi kwa Abdulhalim Humud ambaye alimrudishia mfungaji huyo akafumua shuti kali la chini likajaa nyavuni pembezoni mwa lango kulia.
Bocco ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Simba SC leo, alimtoka Amir Maftah upande wa kulia wa Uwanja na kuingia ndani kabla ya kutoa krosi fupi kwa Kipre aliyemtungua Kaseja na kuipatia Azam bao la pili dakika ya 35.
Simba ilipata bao lake la kwanza dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza, baada ya kutimu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, mfungaji Daniel Akuffo kwa penalti, baada ya Said Mourad kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kipindi cha pili Simba walirudi na nguvu zaidi na kuamua kushambulia kwa mipira ya pembeni, ikiwatumia Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi ambao walikuwa wakibadilishana reli.  
Kwa staili hiyo, haikushangaza Simba ilipotumia dakika 45 za mwisho kwa kufunga mabao mawili yaliyowatoa nyuma kwa 2-1 na kuibuka kidedea kwa ushindi wa 3-2.
Emanuel Okwi alimchambua kama karanga Erasto Nyoni na kuingia ndani kabisa akiwatoka mabeki wengine wa Azam, kabla ya kuujaza mpira nyavuni kwa shuti kali na Kazimoto akamaliza kazi dakika ya 78.
Kwa ujumla katika mchezo huo, Azam ilitawala kipindi cha kwanza na ilikosa mabao mawili zaidi ya wazi kupitia kwa Himid Mao na Kipre, lakini kipindi cha pili Simba walitawala mchezo na kama wangekuwa makini, nao wangeweza kuvuna mabao zaidi.  
Naibu Waziri wa Kazi, Makongoro Mahanga alimkabidhi ngao Nahodha wa Simba, Juma Kaseja baada ya mechi hiyo, ambaye alikwenda kushangilia na wachezaji wenzake na mashabiki wa timu hiyo.    
Hii ni mara ya pili mfululizo Simba wanatwaa Ngao, baada ya mwaka jana pia kuibeba wakiifunga Yanga 2-0.
Aidha, hiyo inakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa kihistoria nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.

 
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu, Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na kiraka Shomari Kapombe. 
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Paschal Ochieng/Juma Nyosso dk 73, Shomary Kapombe, Ramadhan Chombo/Amri Kiemba dk69, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Daniel Akuffo/Abdallah Juma dk64, Haruna Moshi na Emanuel Okwi.
Azam FC; Deo Munishi ‘Dida’, Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Mourad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Ibrahim Mwaipopo/Salum Abubakar dk 58, Himid Mao, John Bocco, Abdi Kassim/Kipre Michael Balou dk 69 na Kipre Herman Tchetche/Zahor Pazi dk 82.


11 wa Simba walioanza leo

11 wa Azam walioanza leo

Bao la kwanza la Azam

Bao la kwanza la Azam

Azam wanashangilia bao la kwanza

Hatari kwenye lango la Simba

Hatari kwa kwenye lango la Simba, Kaseja chini kule

Himid Mao alikaribia kufunga baada ya kumvisha kanzu Kaseja, lakini mpira ukapaa juu kidogo

Kipre Tchetche akiwatoka mabeki wa Simba

Azam wanashambulia

Hatari kwenye lango la Simba


John Bocco anamtoka Maftah

Bocco anatoa pasi ya bao

Humud anampongeza Bocco kufunga

Bocco anampongeza Kipre kuitumia vema pasi yake

Mashabiki nwa Simba

Akuffo akiwa amembeba Okwi baada ya kufunga bao la kusawazisha


Abdallah Juma akumpongeza Kazimoto kufunga la ushindi, Anyeipa mgongo kamera ni Nyosso 

Kazimoto akiwapungukia mkono mashabiki wa Yanga baada ya kufunga la ushindi. Kulia Nyosso na kushoto Abdallah Juma

Mashabiki wa Simba wakiwa na jezi iliyoandikwa Kagawa Ngassa

Kushoto Kaseja, kulia Ngassa na Akuffo wakicheza kiduku 

Ngassa akishangilia kwa staili ya aina yake

Nyamlani akimpa mkono wa pongezi Akuffo. Anayemfuatia ni Waziri Mahanga, akiwasubiri Ngassa na Komabil Keita

No comments:

Post a Comment