Tuesday, November 27, 2012

KIPA LA MAANA KULIFUNGA KWA MBINDE TAYARI KUTUA SIMBA SC


Abbel Dhaira


Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
KIPA namba moja wa Uganda, Abbel Dhaira anayedakia klabu ya I.B.V FC ya Iceland, amesema kwamba yuko tayari kuhama Ulaya na kuja Tanzania kuchezea klabu ya Simba, iwapo watafika dau lake.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Dhaira alisema kwamba mwaka jana Simba walimfuata, lakini wakashindwa kumalizana naye na akaendelea kucheza Ulaya.
Hata hivyo, Dhaira ambaye ni miongoni mwa makipa bora katika ukanda huu kwa sasa, alisema anawapa nafasi nyingine Wekundu hao wa Msimbazi.
“Nina siku tatu tu kabla ya kumaliza mkataba wangu na klabu yangu. Kabla ya kuingia nao mkataba mpya, nawapa nafasi nyingine Simba SC,”alisema, Dhaira ambaye aliibukia Express ya hapa mwaka 2006 kabla ya 2008 kuhamia U.R.A. pia ya hapa, ambayo aliichezea hadi 2010 alipohamia Ulaya.
Hata hivyo, Dhaira hataonekana tena kwenye michuano ya mwaka huu ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge baada ya kuumia jicho katika mechi ya kwanza dhidi ya Kenya, Jumamosi.
Akilizungumzia hilo, Dhaira alisema imemsononesha sana kwani alijitoa kwa ajili ya kuja kuisaidia nchi yake kwenye mashindano haya, lakini kwa bahati mbaya ameumia.
“Ni mambo ya kawaida katika mchezo, nashukuru timu yetu ni nzuri na kuna wachezaji wengine wazuri na ndiyo maana imeendelea kufanya vizuri,”alisema.
Simba SC kwa sasa inasaka kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza, Juma Kaseja ambaye amekuwa akisotoshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema hataki tena kuchezea Simba.
Lakini pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.

No comments:

Post a Comment