Tuesday, December 11, 2012

EL-Merreikh yatoa tamko juu ya kupotea kwa Ngassa


Songombingo la kupotea kwa mchezaji Mrisho Ngassa bila taarifa yoyote kwa vilabu vyake vya Simba na Azam FC, na klabu inayomtaka kumsajili ya El Merreikh ya Sudan limechukua sura mpya jioni hii baada ya msemaji wa klabu ya El Merreikh kuzungumza na kipindi cha Sports Extra cha Clouds FM.

Akizungumza na Shaffih Dauda, shekhe Idrissa amesema kwamba El Merreikh imeshakubalina kimsingi na vilabu vya Azam FC na Simba SC na mchezaji na kilichokuwa kimebakiwa na kutia saini kwa mikataba pamoja na kufanya vipimo vya afya ili mchezaji huyo aweze kujiunga na timu hiyo tajiri ya Sudan, lakini muda mfupi baada ya kufika Dar es Salaam mchezaji huyo amekuwa mafichoni - akiwa hapokei simu na muda mwingine anazima bila kutoa taarifa zozote kwa vilabu husika.

"Mrisho Ngassa tulikuwa tumeshafanya nae mazungumzo vizuri na tukakubaliana na ikabakia kumalizana na vilabu vya Simba na Azam, lakini sasa tukiwa tayari tumemalizana na vilabu mchezaji mwenye amekuwa akifanya vitendo visivyo vya kistaarabu, simu yangu hapokei na muda mwingine anaaizima kabisa. Hili sio jambo zuri kabisa kwake na kwa mpira wa Tanzania kiujumla. Anaharibu sifa ya wachezaji wenzie wa kitanzania, ni vizuri angepokea simu na kutueleza kama dili linawezekana au tofauti, kuliko kutuacha sisi tukipoteza muda kuwepo hapa Tanzania. Kwa tabia hii ya Ngassa tumefikia maamuzi ya kwamba mpaka kesho asubuhi kama mchezaji atakuwa hajapatikana then tutasitisha uhamisho wa mchezaji huyu na kuangalia sehemu nyingine mbali na Tanzania." - Alimaliza Shekhe Idrissa.

Taarifa zilizoenea ni kwamba Ngassa hataki kwenda El Merreikh baada ya kushawishia na viongozi wa Kulwa ili aendelee kuwepo Simba mpaka mkopo wake utakapoisha mwakani na aweze kujiunga na klabu hiyo yake ya zamani.

No comments:

Post a Comment