Wednesday, December 5, 2012

NGASSA ATUA EL MERREIKH KWA DOLA 75,000

Ngassa; Sasa mutu ya fweza
BIASHARA imeisha. Azam FC imemuuza Mrisho Khalfan Ngassa kwa dola za Kimarekani 75,000 kwenda El Merreikh ya Sudan ambako amesaini mkataba wa miaka miwili, utakaomuwezesha kulipwa mshahara wa dola za Kimarekani 4,000 kwa mwezi huku naye akilipwa dola 50,000 za kusaini.
Awali, Merreikh walitaka kumpa mkataba wa miaka mitatu Ngassa wenye thamani ya dola 100,000, lakini wakala wake Alhaj Yussuf Said Bakhresa akakataa akisema utambana mchezaji wake aking’ara na kutakiwa na klabu nyingine.
Sasa Ngassa baada ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwishoni mwa wiki hii, atakwenda Sudan kufanyiwa vipimo tayari kujiunga na klabu hiyo, ambayo ni jambo la kawaida kucheza hatua ya makundi ya michuano ya klabu Afrika.
Azam FC imesema imeweka mbele maslahi ya mchezaji na taifa kwa ujumla katika maamuzi ya kumuuza Sudan, kutoka Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo. “Hii timu (Merreikh) kila mwaka inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, maana yake huyu mchezaji atakwenda kupata maendeleo na kuja kuisaidia zaidi Tanzania katika mashindano ya kimataifa,”alisema kiongozi mmoja wa Azam.  
Alipoulizwa kuhusu Simba SC aliyokuwa anaichezea klabu hiyo, kiongozi huyo alisema wao walimtoa kwa mkopo Ngassa kwenda kwa Wekundu wa Msimbazi hadi Mei 31, mwakani na mkataba wao ndio unasema hivyo.
“Sisi tuliwapa Simba huyu mchezaji kwa mkopo hadi Mei 31 na wakatupa Sh. Milioni 25, ila tuko tayari kuwarudishia fedha zao walizota, lakini huyu mchezaji ni mali yetu  na hata TFF wanatambua hilo, na tumekwishamuuza Merreikh,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu Simba kusaini mkataba mpya na Ngassa, alisema; “We uliona wapi dunia nzima timu inapewa mchezaji kwa mkopo halafu inamsainisha mkataba? Simba lazima ifike wakati waache kurudia makosa, haya ndio mambo ya Mbuyu Twite sasa,”alisema kiongozi huyo wa Azam.
Katika kukamilisha mauzo ya mchezaji huyo, kiongozi wa Marreikh akiwa Dar es Salaam mbele ya viongozi wa TFF na Azam, alipigiwa simu Ngassa aliye hapa Kampala, Uganda na kuhusishwa katika dili hilo, naye akakubali ndipo mambo yakamalizwa.
Aidha, Azam wameomba TFF ihakikishe kunakuwa na ulinzi katika kambi ya timu ya taifa mjini hapa, ili Simba wasimfanyie vurugu Ngassa na kumvuruga kisaIkolojia, wakati ndiyE tegemeo la timu katika kampeni ya kutwaa Kombe la Challenge mwaka huu mjiini hapa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe akizungumza kutoka Dar es Salaam, alisema kwamba watawapeleka mahakamani Azam kwa kitendo cha kumuuza mchezaji wao kinyume cha sheria.   

 
“Haiwezekani wamuuze wao, wakati wao walituuzia huyu mchezaji na sisi tuna mkataba ambao tulisaini nao, hii ni kinyume cha sheria na sisi tutawapeleka mahakamani,”alisema Hans Poppe ambaye anatua kesho mjini hapa.
Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.

Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.

No comments:

Post a Comment