NDOTO za Tanzania Bara kurejea nyumbani na Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge zimeyeyuka baada ya usiku huu kufungwa na wenyeji Uganda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Kwa matokeo hayo, Uganda itamenyana na majirani zao na wapinzani wao wakubwa, Kenya katika fainali Jumamosi, ambao katika mchezo wa kwanza waliitoa kwa mikwaju ya penalti 4-2 Zanzibar, kufuatia sare ya jumla ya 2-2 ndani ya dakika 120.
Wachezaji wa Stars wakiwa hawaamini kilichotokea |
Zanzibar na Bara zitamenyana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu siku hiyo hiyo ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Namboole.
Hadi mapumziko, Uganda walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Emmanuel Okwi dakika ya 11, baada ta kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na kipa wake, Hamza Muwonge na kufumua shuti kali la umbali wa mita 19, ambalo lilimshinda kipa Juma Kaseja.
Baada ya bao hilo, Okwi aliumia na kutoka nje dakika ya 36 nafasi yake ikichukuliwa na Hamisi Kiiza.
Uganda ndio waliouanza mchezo huo kwa kasi na kulitia misukosuko lango la Stars kwa takriban dakika 10 mfululizo, lakini baada ya hapo timu hizo zikaanza kushambuliana kwa zamu.
Timu zote zilikuwa zikishambulia kutokea pembeni, lakini Uganda ndio walioonekana kuzalisha mashambulizi ya hatari zaidi.
Kipa na Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alitoka uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza akilaumiana na mabeki wake kwa kufungwa bao la kutanguliwa.
Kipindi cha pili, Waganda walirudi na moto wao tena na kufanikiwa na kupata bao la pili dakika ya 51, safari hii Robert Ssentongo akimtungua Kaseja, baada ya mabeki wa Stars kudhani ameotea.
Pamoja na kufungwa bao la pili, Stars waliendelea kucheza kwa juhudi, ingawa Waganda waliendelea kutawala mchezo.
Mpira uliotemwa na Juma Kaseja kufuatia shuti la Moses Oloya, ulimkuta Ssentongo dakika ya 71 akaukwamisha nyavuni na kuipatia The Cranes bao la tatu. Kutoka hapo, hali ilikuwa mbaya kwa Stars.
Zikiwa zimesalia dakika tano mchezo kumalizika, taa za Uwanja wa Mandela zilizimika, lakini baada ya jitihada za pamoja za FUFA, CECAFA na uongozi wa Uwanja, ziliwaka baada ya dakika saba na mchezo kuendelea hadi filimbi ya mwisho.
Uganda Cranes : Hamza Muwonge, Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi, Henry Kalungi, Isaac Isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito, Moses Oloya, Robert Ssentongo, Emanuel Okwi/Hamisi Kiiza dk36 na Joseph Ochoya/Brian Majwega dk79.
Kilimanjaro Stars : Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Franko Domayo, Amri Kiemba, Salum Abubakar/Athumani Iddi dk63, Mwinyi Kazimoto, John Bocco na Mrisho Ngassa.
No comments:
Post a Comment