Tuesday, January 15, 2013

Mbatia akatisha ziara Mtwara

MWENYEKITI wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amekatisha ziara yake mkoani Mtwara, baada ya juzi kunusurika kipigo kutoka kwa baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wake, Uwanja wa Mashujaa.

MWENYEKITI wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia

Mbatia na wabunge wake, Moses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini), waliokolewa na polisi baada ya kujifungia ofisi za chama hicho Wilaya ya Mtwara Mjini kuanzia saa 11:45 jioni hadi saa 1:17 usiku.

Wananchi waliizingira ofisi hiyo, huku wakiimba nyimbo za kumshtumu Mbatia kuwa, ni mamluki aliyetumwa na Serikali kulainisha msimamo wao kuhusu gesi inayovunwa Kijiji cha Msimbati kutopelekwa Dar es Salaam.

Kadiri jua lilivyokuwa linazama na giza kutanda, ndivyo hali ya usalama wa viongozi hao ilivyozidi kuwa tete, wananchi walianza kutupia mawe ofisi hiyo na wengine kujaribu kuvunja mlango kwa kurusha vitu vinavyosadikiwa ni mabomu ya kuulia samaki baharini.
Milipuko mithili ya bomu ilisikia mara mbili mlangoni hapo na miale ya moto kuonekana, kitendo ambacho kiliashiria usalama wa Mbatia na viongozi wengine kuwapo shakani iwapo polisi wasingejitokeza mapema kuwaokoa.


Mabomu ya machozi yaliyorushwa na polisi, yalitosha kuwatawanya wananchi hao na Mbatia na wenzake kupata ahueni ya kutoka ofisini humo usiku.Kutokana na tatizo hilo, Mbatia amekatisha ziara yake na kurejea Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mtwara Mjini, Uledi Abdallah alisema kwamba viongozi hao jana walipaswa kufanya mkutano mkubwa Kijiji cha Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa, lakini kutokana na hali iliyojitokeza uongozi huyo umekatisha ziara yao.

“Nimesikitishwa sana, nimefadhaishwa sana na tukio la jana…Ilikuwa leo (jana) aendelee na ziara yake kule Msimbati, lakini kutokana na sababu za usalama amekatisha,” alisema Abdallah na kuongeza:

“Umoja wa vyama tunasema tukio lile ni la kupandikiza, ili tuonekane tunahatarisha usalama wa wananchi… Wanataka kuishawishi polisi watunyime vibali vya kufanya mikutano ili gesi waichukue kwa urahisi.”

Hoja inayozungumzwa kuwa ni kichocheo ya vurugu hizo ni kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa mbunge na kwamba, wananchi wanaamini hawezi kupingana na msimamo wa ‘bosi’ wake.

No comments:

Post a Comment