Tuesday, January 29, 2013

Profesa Ndulu ataka BoT isiingiliwe na wanasiasa

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu amependekeza Katiba Mpya iweke kinga ambayo itailinda benki hiyo ili ifanye kazi zake bila kuingiliwa na mambo ya kisiasa.

Aidha, amependekeza Katiba Mpya itenganishe mamlaka zinazotoa na zile zinazotumia fedha ili kila moja ifanye kazi zake kwa kujitegemea, huku pia akitaka kinga zinazolinda shughuli za kibenki zitambulike kikatiba na si kuwepo kwenye sheria za Bunge.

Alisema benki zinapaswa kutoa fedha kwa kiwango maalumu bila kuzizidisha kwa ajili ya kuimarisha uchumi.
Akizungumza Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya kuwasilisha maoni ya BoT kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Ndulu alisema umefika wakati BoT ikajengewa uwezo wa kufanya shughuli zake bila kuingiliwa na wanasiasa.

Profesa Ndulu alisema endapo BoT itawekewa kinga itakuwa na uwezo wa kufanya kazi zake vizuri zaidi.

Mamlaka za fedha
Kuhusu mamlaka za fedha Profesa Ndulu alisema: “Tumependekeza kwamba Katiba ijayo iwe na kifungu kitakachotenganisha mamlaka zinazohifadhi fedha na zinazotumia fedha ili kila moja iweze kufanya kazi zake kwa kujitegemea.”Pia, Profesa Ndulu alipendekeza Katiba Mpya iwe na kinga itakayolinda shughuli za kibenki itakayotambulika na siyo kuwapo kwenye sheria za Bunge.


Mbowe aiasa Tume
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameiasa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kusimamia maoni ya wananchi katika kukamilisha mchakato wake wa upatikanaji wa Katiba Mpya ili kuondoa malalamiko.

Mbowe alisema kuandika Katiba ni jambo moja na kuipitisha ni jambo jingine, hivyo kuitaka iandae katiba itakayokubalika na wananchi wengi.

“Kwa kuwa Chadema tunaamini wananchi ndiyo wenye uamuzi wa kila kitu, hivyo endapo tume itakuja na katiba ambayo hatukuitarajia tutarudi kwa wananchi na kuwaeleza ili kutoikubali,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Katika mabadiliko hayo, pia tunaomba Katiba ije na muundo wa Serikali tatu ili Tanzania bara iwe na mamlaka yake kama ilivyo kwa Zanzibar ambao wana wimbo wao wa taifa, bendera yao, Katiba yao, Bunge lao, Rais na Makamu wa Rais wao sasa tunabembeleza nini?”

Alisema katika uchaguzi ujao, Chadema hakitakubali kushiriki endapo Katiba hiyo haitatambua kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

“Tunataka Tume Huru ya Uchaguzi na kama haitakuwa hivyo tutarudisha uamuzi kwa wananchi na kuingia barabarani kuidai,” alisema.

No comments:

Post a Comment