Thursday, January 17, 2013

Unyama wa polisi kwa wanafunzi IFM ulaaniwe

TUNASHINDWA kupata maneno sahihi kuelezea unyama na ukatili wa kutisha uliofanywa na Jeshi la Polisi juzi kwa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) walipoandamana jijini Dar es Salaam kulishinikiza jeshi hilo kuwapa ulinzi, kutokana na makundi ya wahuni kuhatarisha usalama wa wenzao wanaoishi Kigamboni, wilayani Temeke kwa kuwapora, kuwabaka na hata kuwalawiti.Picha za magazeti ya jana na juzi ziliwaonyesha polisi waliosheheni silaha za kivita wakifanya unyama huo kwa kuwapiga na kuwajeruhi vibaya wanafunzi waliokwenda katika Kituo cha Polisi cha Kigamboni kulalamikia kitendo cha polisi kutochukua hatua dhidi ya makundi ya wahuni wanaowatesa na kuwadhalilisha wanafunzi hao.Picha hizo za kuhuzunisha na kughadhabisha zilionyesha pasipo kuacha shaka kwamba Jeshi la Polisi siyo chombo cha kulinda raia na mali zao kama inavyodhaniwa, bali ni mabaki ya jeshi la kikoloni lililorithi utamaduni wa kutesa na kupora haki za wananchi. Katika picha hizo, polisi walionekana wakifanya vitendo vya kikatili kwa wanafunzi hao waliokuwa wakiandamana kwa amani. Baadhi ya picha zilionyesha polisi wakiwatesa wanafunzi wa kike kwa kuwapiga virungu vichwani, huku wanafunzi hao wakilia na kusaga meno.Picha hizo zilikuwa kumbukumbu tosha ya polisi wa Kikaburu walivyokuwa wakitesa wazalendo huko Afrika ya Kusini kabla nchi hiyo haijapata uhuru. Kosa la wazalendo hao, kama lilivyokuwa kosa la wanafunzi hao wa IFM juzi ni kudai haki zao za kiraia za kukataa maisha ya mateso na udhalilishwaji ili waishi maisha ya utu, heshima na amani. Badala ya polisi kusikiliza hoja zao na kuahidi kuzifanyia kazi mara moja, walitunisha misuli na kuwapa kipigo kama wafanyavyo kwa majambazi na wahalifu sugu.


Inasikitisha kuona kwamba kila mara polisi wanapozima maandamano wanakuwa kama wanyama wasiokuwa na akili timamu. Hawaonyeshi kuchukua tahadhari yoyote au kuonyesha ubinadamu kwa watu hao wanaodai haki zao kwa amani. Hawaonyeshi weledi wa kazi zao, bali wanatumia nguvu na mitulinga na kuvunja haki za binadamu kwa kusababisha mateso na maumivu kwa watu hao.


Madai ya wanafunzi wa IFM yalikuwa sahihi kwa vigezo vyovyote vile. Maandamano yao yalikuwa na lengo la kuwapa moyo na kuwafariji wenzao waliokuwa wakiporwa fedha na mali zao kila kukicha, mbali na kudhalilishwa kwa kubakwa na kulawitiwa, huku polisi wakishindwa kuchukua hatua dhidi ya makundi ya wahuni yaliyokuwa yakifanya vitendo hivyo, hata baada ya kupewa taarifa kuhusu wahalifu hao. Tungetegemea Polisi hao wawafariji wanafunzi waliodhalilishwa badala ya kuwapa kipigo.


Sisi tunalaani kwa nguvu zote unyama huo uliofanywa na polisi.Tunapendekeza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya jeshi hilo, kwani matukio ya mauaji, mateso na unyanyasaji wa raia wasiokuwa na raia ambayo yamekuwa yakifanywa na polisi katika miezi ya hivi karibuni ni ushahidi tosha kwamba jeshi hilo limekosa mwelekeo na linapaswa lidhibitiwe ili liheshimu sheria na haki za binadamu na kuzingatia dhana ya utawala bora.


Tunawataka viongozi na wanafunzi wa IFM waache woga, wasimame kidete na kupigania haki za wenzao waliotiwa aibu na hofu na magenge hayo ya wahuni huko Kigamboni. Ni matumaini yetu kwamba polisi watatimiza wajibu wao kwa kuyadhibiti magenge hayo na kuyafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.

No comments:

Post a Comment