Wednesday, January 9, 2013

UWT waukimbia mkutano wa Mama Salma Kikwete

BAADHI ya wanachama wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, wamesusia kushiriki kikao kilichoitishwa na mke wa Rais wa Tanzania, mama Salma Kikwete, kwa madai ya kukarishwa na kitendo cha wanachama wa CUF kuhudhuria..

Habari kutoka Wilayani humo na kuthibitishwa na baadhi ya wanachama wa CCM na CUF waliokuwa wamejitokeza kuudhuria kikao hicho, zinaeleza kuwa tukio hilo limefanywa na wanachama hao jana mchana, katika Ukumbi wa Jumba la Maendeleo mji mdogo wa Masoko.

Mama Salama Kikwete
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya walioudhuria kikao hicho, walisema wanawake hao wa CCM walichukuwa uamuzi wa kususia kikao hicho, kupinga kitendo cha uongozi wa Serikali wilayani humo, kuwashirikisha wenzao wa CUF akiwemo aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Mwanawetu Said Zarafi.

Aidha, walisema kufuatia mtafaruku huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Abdallah Hamisi Ulega, alipowasihi wanachama hao, hawakuwa tayari kutii ombi la kiongozi huyo wa wilaya.


Akizungumza na gazeti hili, mbunge wa zamani wa viti maalum Mkoa wa Lindi, Mwanawetu Said Zarafi, amekiri kuwapo kwa mtafaruku huo, na kueleza ulitokana na kukasilishwa na kitendo cha mke wa Rais, mama Salma Kikwete kuwataka wanawake wote wakiwamo na wajasiriamali bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, dini au rangi.

Zarafi alisema kutokana na mwaliko huo, yeye pamoja na vikundi vinne vya wajasiriamali wa kike, ambao ni wanachama wa CUF wilayani Kilwa wakaudhuria kwenye kikao hicho.

Alisema kitendo cha wao kutinga ndani ya ukumbi huo, wanachama hao wa kike wa CCM, wakatangaza vita kwa kuwataka watoke nje kwani kikao hicho hakiwahusu, na pale wasipotekeleza amri hiyo watafunga mlango tayari kwa kuzichapa kavukavu.

“Wakati vitendo hivyo vinafanyika mgeni rasmi, mama Salma Kikwete alikuwa bado hajawasili ukumbi humo,”alisema Mbunge huyo wa zamani.

Mwanawetu alisema kufuatia kitendo hicho, yeye na baadhi ya wanawake walikwenda nyumbani kuchukua kanga kwa ajili ya kupamba tena kwenye meza hiyo.

“Kwa sababu wengi walisusia, tulilazimika kwenda kwenye nyumba mbalimbali na kuwachukua wanawake wengine,”alisema Mshiriki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Esha Ally.

Aidha, gazeti hili lilipomtafuta mkuu wa wilaya hiyo,Abdallah Hamisi Ulega, ili kupata kauli yake hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita bila ya kupokelewa.

Mke wa Rais, mama Salma Kikwete alikuwa na ziara ya siku moja katika wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, ambapo alikuwa na mazungumzo na akina mama wakiwemo na wajasiriamali,na kuwataka wawe na upendo pamoja na mshikamano wa kweli kwa lengo la kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Pia aliwataka wajitokeze kugombea uongozi katika ngazi mbalimbali, zikiwemo udiwani, ubunge na urais, huku akiwasisitiza kumpa ushirikiano kwa mwanamke mwenzao pale atakapojitokeza kuwania nafasi bila ya kujali itikadi zao zikiwemo za siasa, dini, rangi au kabila lake.


source:http://www.mwananchi.co.tz/habari/-/1597578/1661140/-/vk4wpd/-/index.html

No comments:

Post a Comment