Patashika langoni mwa Yanga FC |
YANGA
SC imejitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia
ushindi wa bao 1-0 jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi
ya Azam FC.
Matokeo
hayo, yanaifanya Yanga itimize pointi 39, baada ya kucheza mechi 17,
hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 36
ambayo pia imecheza mechi moja zaidi.
Hadi
mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa kitaalamu na
kiungo Haruna Niyonzima aliyepokea pasi ya Jerry Tegete. Lilikuwa
bao tamu, lililotokana na mpangilio mzuri wa shambulizi, Yanga
wakigongeana pasi kutokea nyuma hadi kwenye eneo la hatari la Azam.
Yanga wakishangilia bao la Haruna Niyonzima |
Mshambuliaji
Jerry Tegete leo bahati haikuwa yake, kwani aliikosesha Yanga mabao ya
wazi katika dakika za 40, 44 na 61, akiwa kwenye nafasi nzuri za
kufunga.
Azam nao walipoteza nafasi tatu nzuri za kufunga, mbili kupitia kwa Kipre Tchetche dakika ya 59 na 61 na nyingine John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 67.
Katika
mchezo huo, kipindi cha kwanza Yanga walitawala zaidi na kufanya
mashambulizi mengi ya hatari, lakini kipindi cha pili Azam ndio
waliotalawa zaidi na kukaribia kusawazisha. Katika
kupunguza kasi ya Azam, kipa wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’ alikuwa
akijiangusha angusha mara kwa mara ili kupoteza muda, kiasi cha kupewa
kadi ya njano na refa Hashim Abdallah.
Wachezaji wa Azam wakiongozwa na John Bocco ‘Adebayor’ walimvamia refa Hashim baada ya mchezo, wakimlalamikia kumaliza mchezo kabla ya muda. Kutokana na tafrani hiyo, ilibidi Polisi waingie uwanjani kuwatoa marefa chini ya ulinzi wao na walipofika kwenye mlango wa kuingilia vyumbani mwao, mashabiki wa Simba walianza kuwatupia chupa.
Kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall alianza kwa kuwapongeza Yanga na akasikitika hawakucheza vema kuweza kushinda, hususan kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili walijaribu, ingawa alisema wapinzani wake walikuwa bora katika ulinzi.
Kocha
wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alisema vijana wake walicheza vema
kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili walipoteza mwelekeo na
akashukuru mno bao la Niyonzima limempa pointi tatu.
Kikosi
cha Yanga SC ; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar
Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’,
Simon Msuva, Frank Domayo, Jerry Tegete/Didier Kavumbangu, Hamisi
Kiiza/Said Bahanuzi na Haruna Niyonzima.
Kikosi cha Azam FC ; Mwadini Ally, Kipre Balou/Jabir Aziz, Waziri Salum, Joackins Atudo, David Mwantika, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar, John Bocco, Kipre Tchetche, Humphrey Mieno na Khamis Mcha ‘Vialli’/Seif Abdallah.
No comments:
Post a Comment