WANACHAMA na mashabiki wa soka nchini wameapa kuandamana na kwenda Mahakamani kuzuia kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), baada ya Kamati ya Rufaa ya Shirikisho hilo kumuengua mgombea wa nafasi ya urais, Jamal Emil Malinzi.
Aidha, wanachama hao kutoka klabu za Simba, Yanga na Azam wamemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kuingilia kati suala la kuenguliwa kwa Malinzi kwani limefanywa kwa chuki binafsi likiwa na lengo la kumbemba mpinzani wake, Athumani Jumanne Nyamlani.
Jamal Malinzi |
Wakizungumza na Waandishi wa habari leo, pamoja na kupinga kuondolewa kwa Malinzi, wametoa siku tatu kwa TFF kumrejesha katika kinyang’anyiro hicho, kinyume na hapo watakwenda kudai haki yao Mahakamani. Mmoja ya wadau hao Kaisi Edwin alisema kwamba kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) chombo cha mwisho cha maamuzi ni Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Michezo (CAS) lakini TFF haijaelekeza baada ya kamati ya Rufaa chombo kipi kinaweza kutoa suluhu ya masuala kama hayo.
Alisema walitaka kupata changamoto mpya ya uongozi kupitia kwa Malinzi lakini kitendo cha kumuengua kinaonesha ni jinsi gani wanavyotaka kuendelea kuwa na watu wasiotaka maendeleo ya soka. “Ni bora tufungiwe na FIFA, tunajua maslahi wanayoyapata TFF na tutatoa uozo wote...kwa hili hata damu itamwagika na kwa gharama yoyote tutahakikisha uchaguzi haufanyiki kama wasipomrejesha Malinzi labda waende kufanyia Geneva,”aliusema Kaisi.
Naye Suleiman Kato alisema anashangazwa na kamati ya Rufaa kumuengua Malinzi kwa madai ya kutokuwa na uzoezfu wakati alipitishwa kugombea uchaguzi wa mwaka 2008 inagawa alishindwa kwa kura chache na rais wa sasa wa TFF, Leodger Tenga. “Malinzi pia ni mwenyekiti wa chama cha soka Kagera sasa iweje apitishe kugombea huko na mpaka anapata kiti hicho na hii leo mseme hana uzoefu na uongozi wa soka, kinachoonekana hapa ni kutaka kudidimiza soka la Tanzania, hilo hatulikubali,”alisema.
Mdau mwingine, Mgeni Ramadhan ‘Dogo Macho’ alisema inaonesha waziwazi wanataka viongozi kwa ajili ya maslahi binafsi kitu ambacho si sahihi kwani Watanzania wanaopenda soka wanataka maendeleo na si viongozi maslahi.“Naamini Rais Kikwete ambaye ni mpenda michezo atasikia kilio hiki na kuingilia kati, kuna watu wapo kwa ajili ya kubebwa, huyo Nyamlani anatoka Kusini, kuna mwanakamati mmoja Murtaza Mangungu ambaye ni Mbunge anambeba, pia kuna mwingine aliwahi kuwa Hakimu wa Temeke na Nyamlani akiwa karani wake,”alisema.
Kwa upande wake, mdau mwingine Said Bakari alisema kuwa wataanza kuonesha hasira zao kuanzia leo kwenye uwanja wa Taifa kwenye mechi baina ya Yanga na African Lyon, kabla ya kuendelea na hatua yao katika michezo ya kimataifa ya timu za Simba na Azam wikiendi hii. “Huyu Nyamlani anabebwa, kwani tunajua Mwenyekiti wa Kamati alikuwa rafiki yake wakati akiwa Hakimu Temeke yeye alikuwa karani, Mangungu naye pamoja na kumpigia debe ni jirani na baba yake Nyamlani,”alisema.
Wadau hao kwa pamoja wamepaza sauti hizo baada kamati ya Rufaa ya TFF kumuengua Malinzi katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu ambapo kwa mujibu wa ratiba kampeni zinatarajiwa kuanza leo.
Katika hatua nyingine, Malinzi kesho anatarajiwa kuzungunmza na waandishi wa habari kuhusina na sakata hilo.
No comments:
Post a Comment