Thursday, March 14, 2013

Polisi watano kortini wizi wa Sh150 milioni

Maofisa watano wa Jeshi la Polisi nchini wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na shtaka la wizi wa Sh150 milioni. Akiwasomea hati ya mashtaka yanayowakabili, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benard Kongora aliwataja washtakiwa hao kuwa ni sajenti Dancan Mwasabila (43) Koplo  Geofrey (39).


Wengine ni Koplo Rajabu Nkumkwa (46), Koplo Kawanani  Hamphrey (34) pamoja na Koplo Kelvin Mohamed (44). Kongora alidai kuwa Desemba 18, 2012 katika eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala,  washtakiwa hao kwa pamoja waliiba fedha taslimu Sh150 milioni mali ya Mire Artan Ismail.

Washtakiwa wote walikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Hakimu Mchauru aliwataka washtakiwa hao kila mmoja kusaini bondi ya Sh5 milioni na kuwasilisha fedha taslimu Sh15 milioni  ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha. Mbali na masharti hayo ya dhamana, pia kila mshtakiwa alitakiwa  kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika  ambao kila mmoja wao angesaini bondi ya Sh5 milioni. Kesi hiyo itatajwa mahakamani hapo Machi 27.

No comments:

Post a Comment