Uongozi wa Tanzania Houston Community
(THC) unapenda kukanusha taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa mitandaoni ya
kwamba ubalozi wa Tanzania nchini Marekani chini ya Mh. Balozi Wilson Masilingi
haukufanya lolote wakati jumuiya yetu ilipopatwa na misiba miwili ya Bw.Henry
Kiherile na Bw.Andrew Nicky Sanga iliyotokea kwa nyakati tofauti mapema mwezi
April mwaka huu.
Uongozi
wa THC unapenda umma utambue kwamba tulipata na tunathamini sana
ushirikiano ulioonyeshwa na kutolewa na ubalozi pamoja na balozi mwenyewe Mh.
Masilingi wakati wa misiba hiyo miwili na hata baada ya shughuli hizo za misiba
kumalizika.
Marehemu Andrew Sanga ( kushoto ) na Marehemu Henry Kiherile ( kulia ) enzi za uhai wao |
Baadhi ya mambo yaliyofanywa na balozi ni
kuwatafuta viongozi wa jumuiya THC na kuzungumza nao mapema baada ya misiba hiyo
kutokea (balozi alitutafuta viongozi na si vinginevyo) ambapo alizungumza na
Rais wa jumuiya Bw. Daudi Mayocha kwa simu na Katibu mkuu wa jumuiya Bw. Michael Ndejembi na kuwapa pole
kwa niaba ya familia na jumuia nzima.
Uongozi unafahamu kwamba sababu za balozi
kushindwa kufika Houston wakati wa misiba hiyo ni yeye kumuwakilisha Mh. Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Magufuli kwenye kongamano la DICOTA
lililokuwa likifanyika jijini Dallas, Texas. Tunatambua pia kwamba nia ya
balozi kuja Houston bado iko pale pale.
Aidha Balozi Masilingi alimtuma afisa
ubalozi Bw. Dismas
Assenga kumuwakilisha katika shughuli za Misa na Kuaga mwili wa marehemu Andrew
Nicky Sanga, ambapo afisa huyo pamoja na mambo mengine alitoa salamu za
rambirambi toka kwa balozi na alikabidhi rambirambi ya $500 kwa kila familia
pamoja na kuzungumza na wafiwa hao kwa
nyakati tofauti.
Kwa taratibu za kiupelelezi Uongozi wa THC
hauwezi kutoa taarifa zaidi ya namna suala hili linavyoshughulikiwa kati ya
vyombo vya usalama nikimaanisha HPD Homicide Department na Ubalozi wa Tanzania
lakini tunatambua kwamba ubalozi unafuatilia kesi zote mbili kwa ukaribu sana.
Uongozi wa THC unasisitiza kuwa hauhusiki
kwa aina yoyote na Waraka (Petition) unaosambazwa kwenye mitandao kumchafua
Balozi Masilingi na ubalozi wetu wa Washington D.C kwa ujumla.
Daudi Mayocha,
Rais wa Jumuiya ya Watanzania Houston
(THC)
thc.leaders@gmail.com
No comments:
Post a Comment