Thursday, November 18, 2021

MPAMBANO WA MASHABIKI WA SIMBA vs YANGA UGHAIBUNI KUFANYIKA HOUSTON THANKSGIVING WEEKEND

 Mpambano wa kukata na shoka wa mashabiki wa timu mahasimu Simba vs Yanga wa Ughaibuni unatarajiwa kufanyika Jumamosi ya wiki ijayo Jijini Houston Texas. Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki kutoka pande mbalimbali Marekani utafanyika kwenye viwanja vya Cullen Park kuanzia mida ya saa 11 jioni. 

Maandalizi ya mpambano huo yamekamilika na wachezaji wa timu zote wako na morali wa hali ya juu kuhakikisha timu zao zinashinda mchezo huo. Mara ya mwisho timu hizo zilikutana jijini hapa mwezi March, 2019 na Yanga SC walikubali kipigo kizito cha mabao 3-0. 




Meneja wa Yanga Himidy Mshale "Aucho" na nahodha wake Charles Ngalawa "Bangala" wamesema wanatarajia kuishushia Simba kipigo kikali cha kufungia mwaka wakiwatumia wachezaji wao chipukizi kama golikipa Shaibu Said, Maneno Ngolo "Makambo" na Ally Abaenya "Mayele". Winga machachari kutoka New York Ebra Nyangaly "Moloko" anategemewa kuwasili Houston akiambatana na meneja wa timu Luke Joe "Engineer" siku ya Ijumaa kwa kutumia ndege ya kukodi.

Naye Meneja wa Simba SC Ughaibuni James Shemdoe "Pablo" akiwa na nahodha wake Rahim Chomba "Bwalya" wamesema kwa upande wao hawana wasiwasi kabisa na majigambo ya Yanga SC kwani kipigo kitakuwa kikali zaidi ya kile cha mwaka 2019. Simba wanajivunia wachezaji wao wenye uwezo wa hali ya juu katika kulisakata kabumbu kama viungo Justice Munissi "Velverde", Iluta Shabaan "Sakho", Thom Juma "Kagere" , Mudhihir Said "Kanoute" na wengineo wengi.

Waamuzi wa mchezo huo kutokea Oklahoma wanatarajia kuwasili asubuhi ya siku ya mchezo ili kuepusha aina yoyote ya figisu za nje ya uwanja.

Nyote mnakaribishwa kushuhudia burudani hii ya kukata na shoka. 




No comments:

Post a Comment