Friday, June 29, 2012


Mgogoro Wa Serikali Na Madaktari Ni Balaa Kwa Taifa

Ndugu zangu,

Nimepitia nilichoandika Februari 4, 2012 juu ya mgogoro wa madaktari na Serikali nikaona ni vema niyarushe tena maandiko yangu yale kama yalivyokuwa, bila kuongeza au kupunguza neno. Maana, kuna ambacho wahusika wanaweza hawakukiona wakati ule, lakini wakakiona sasa. Soma nilichoandika...


Ndugu zangu, 


Mgomo wa madaktari wetu ni habari kubwa. Umeingia sasa kwenye wiki ya pili. Hata kama ungekuwa ni wa siku mbili, bado ungesababisha madhara makubwa kwa nchi. Kwamba sasa una zaidi ya siku kumi na nne ni balaa kubwa kwa nchi yetu.
 

Tafsiri yangu;
 

Uliopo ni mgogoro kati ya madaktari na Serikali. Na kwenye mgogoro kama huu, siku zote, wenye kuathirika zaidi ni wananchi walio wengi.
 

Ni ukweli, kuwa karibu kila Mtanzania anayeamka asubuhi, ama ni mgonjwa au ana ndugu, jamaa au rafiki aliye mgonjwa.
 

Hivyo basi, kuna mamilioni ya Watanzania wenye kutaabika kila siku na maradhi ya aina mbali mbali. Ni Watanzania wenye kutegemea sana huduma ya tiba inayotolewa na madaktari wetu. Na katika nchizetu hizi, daktari ni rafiki muhimu sana wa mwananchi.
 

Ni jambo baya sana, pale Serikali inapoingia kwenye mgogoro na madaktari. Inapoingia kwenye mgogoro na marafiki wa wananchi. Hakuna mahali popote duniani wananchiwakatokea kuwachukia madaktari.
 

Hivyo basi, ni balaa pia pale Serikali inaposhindwa kumaliza tofauti zake na madaktari wa wananchi kwa njia ya mazungumzo na hata kufikia hatua ya madaktari kugoma.
 

Katika nchi zetu hizi, mganga wa tiba aliyesomeshwa kwa fedha za walipa kodi na kwa miaka mingi anahitajika sana. Mganga wa tiba msaidizi anahitajika sana. Na hata kama angelikuwapo Msaidizi wa Mganga Msaidizi wa tiba , naye angehitajika sana. Vivyo hivyo kwa wakunga wakuu na wasaidizi, wauguzi wakuu na wasaidizi wao. Wote hao anahitajika sana.
 

Na katika nchi zetu hizi, Serikali hazipaswi kufikia hatua ya kuwatisha na hata kuwafukuza kazi madaktari. Hilo la mwisho lifanyike tu pale ambapo njia nyingine zote za kumaliza tofauti na kusuluhisha migogoro na madaktari zitakapokuwa zimeshindikana. Na kwanini ishindakane?
 

Tufanye nini sasa?
Taarifa kwamba Kamati ya kudumu ya Bunge inayohusika na masuala ya huduma za jamii imepanga kukutana na madaktari wetu ni hatua njema na ya busara. Maana, katika mgogoro huu taarifa zimekuwa zaidi za upande mmoja; upande wa Serikali. Ni wakati sasa pande zote mbili zikasikilizwa na Kamati hiyo ya Bunge. Ndio, ni wakati pia hata madaktari wetu wakapewa nafasi tuwasikie.
 

Huu si wakati wa kufanya "propaganda" za kisiasa kwenye masuala ya afya za wananchi. Na hata pale Waziri wa Afya alipokaririwa jana Bungeni akitamka kuwa hali ya huduma za mahospitalini zimerejea katika hali yake ya kawaida ni mfano wa ’ Propaganda’ za kisiasa ambazo Watanzania hatuzihitaji kwa sasa. 


Hivi ni hali gani hiyo iliyorejea kwenye kawaida yake kwenye hospitali zetu baada ya mgomo huu wa madaktari unaoendelea sasa? Kwamba askari wetu wa Jeshi la Wananchi wamelazimika kwenda kutibu wagonjwa Muhimbili hiyo haiwezi kuwa ni ’ Hali ya kawaida’. Kwamba madaktari wameripoti lakini hawaonekani mawodini hiyo haiwezi kuwa ’ hali ya kawaida’. Na kama ni kawaida, hivi ni nini tafsiri ya ’ kawaida’?
 

Hapa kuna ukweli unaopaswa kusemwa, na si kitu kingine bali ni ukweli. Watanzania tunataka kujua; ni kwanini watendaji wa Wizara husika wameshindwa kulitatua suala la madaktari wetu na hata kutufikisha hapa tulipo? 


Yumkini, kulikuwa na hali ya kuyapuuzia madai ya madaktari katika hatua za awali. Yawezekana pia watendaji wa Wizara hawakuwa karibu na wawakilishi wa madaktari hao ili kutoa fursa ya kuongea na kutafuta ufumbuzi wa tatizo. Labda ndio maana tumefika mahali sasa mgogoro umekomaa na wahusika kuonyesha hali ya kutunishiana misuli. 


Kuna mahali kosa limefanyika. Ni wapi?
 

Ndio hapa, kuwa hata kama Kamati ya Bunge itafaulu kusuluhisha mgogoro huu, bado Watanzania tutahitaji iundwe Tume huru itakayochunguza namna watendaji wa wizara husika walivyolishughulikia suala hili kwa upande wao.
 

Tume hiyo itusaidie kuupata ukweli mzima ili kama taifa, tujifunze. Na wakati tume kama hiyo itakapokuwa ikifanya kazi yake, itakuwa ni busara, kwa watendaji wakuu wa wizara husika wajiweke pembeni kwa maana ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi huo. 


Kama Tume itabaini kuwa hakukuwa na mapungufu makubwa katika utendaji wao na hususan walivyolishughulikia suala
 
hili la mgogoro na madaktari, basi, itajulikana hivyo, na wana nafasi ya kurudi tena kwenye nafasi za utendaji Serikalini. Inahusu umma kurudisha imani yake kwa Serikali yao. Ndio maana ya umuhimu wa wahusika kupisha pembeni kuruhusu uchunguzi ufanyike. Maana, haitakuwa busara kuliacha suala hili likapita kama yanavyopita mengine ilihali limegharimu maisha ya Watanzania.

Na kubwa zaidi kwa sasa, ni kwa pande zote katika mgogoro huu kutambua; kuwa kwa sasa mvutano unaoendelea hautatoa mshindi, ni kwa vile, katika kilichotokea na kinachoendelea kufanyika sasa, sote, kama taifa, tumeshindwa.
 

Huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye yote, lakini, njia mujarab ya kutanzua mgogoro huu uliopo sasa ni mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana, basi. 


Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika. 


Maggid Mjengwa,
 

Dar es Salaam,
 
Jumamosi, Februari 4, 2012
http://mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment