UKISTAAJABU ya Musa utaona ya Firauni. Mbuzi wa ajabu ajulikanaye kwa jina la ‘Mawimbi’ anafanya vitu ambavyo kwa akili za kibinadamu unaweza usiamini, Amani linamwanika mwanzo mwisho.
Mbuzi huyo anayemilikiwa na Julius Mawimbi Kisena ‘Mawimbi’ mkazi wa Mazizini Ukonga, Dar karibu na Kituo cha Polisi Mazizini ameonekana kuwa kivutio kwa watu wa eneo hilo kutokana na kufanya vitendo vya kibinadamu.
Mapaparazi wetu walimtembelea (Mawimbi) katikati ya wiki hii, nyumbani kwake hapo na kufanikiwa kuongea na ‘bosi’ wake huyo ambaye alikiri mbuzi huyo kuwa na maajabu kibao.
ANAPENDA KULA ‘BATA’
Kwa kawaida mbuzi hujulikana kwa kula majani, lakini ‘Mawimbi’ yeye anapenda kula ‘bata’, vyakula kama nyama choma, nyama iliyopikwa, maandazi, chapati kwa mchuzi, ubwabwa kwa nyama, ugali, chipsi kavu na mihogo ya kukaanga ndiyo mwake.
Ili kudhihirisha hilo, Mawimbi aliwaagiza waandishi waliopiga hodi nyumbani kwake kwenda gengeni kununua chapati ili waamini kile anachokisema juu ya mbuzi huyo mwenye uzito wa kilo 128.
“Ili muamini kweli mbuzi wangu anakula vyakula vya binadamu, nendeni mkanunue chapati mumletee, mtaona atakavyozifuta chapchapu,” aliagiza Mawimbi.
Mapaparazi wetu walikwenda gengeni jirani na makazi ya mbuzi huyo na kununua chapati tano ambapo alipopelekewa, alizifuta kama binadamu anayefungua kinywa kwa chai.
BIA KWA SANA
Mawimbi aliongeza kuwa mnyama huyo anakata kilevi kama hana akili nzuri. Alisema amekuwa akinywa aina zote za bia na ana uwezo wa kunywa za baridi zaidi ya 18 kutokana na uhitaji wake kwa siku bila kupepesuka wala kuwa bwii.
Je, Mawimbi anajuaje kama mbuzi wake ana kiu ya bia?
“Mara nyingi akipata hamu ya bia huenda kwenye baa na kuzungukazunguka hapo mpaka atakapohudumiwa.
“Kama akiwakuta watu wanakunywa huwasogelea na kuwaangalia kwa macho yenye uhitaji. Wanaomfahamu humnunulia na kumwekea kwenye chombo na kumpa. Wasipotekeleza hilo hufanya fujo kwa kupiga kichwa meza za wateja mpaka kuangusha vinywaji vyao,” alisema Mawimbi.
LAKINI MBAKAJI!
Kila kizuri kina kasoro, wakati mbuzi huyo analeta mshangao kutokana na tabia yake hiyo lakini kumbe ana tabia za kubaka wanawake, hasa wale walio kwenye siku zao.
“Tatizo la mbuzi huyu ana tabia ya kubaka wanawake, hasa wale walioko kwenye siku zao,” alisema Mawimbi.
Akaendelea: “Amini usiamini hadi sasa ana kesi 18 za kubaka katika Kituo cha Polisi cha Mazizini. Waathirika wakubwa ni wanawake hao ambao hupita karibu yake.
“Yeye akishasikia harufu ya mwanamke tu huanza kumkimbiza kwa lengo la kupata mambo ya kiutu uzima.”
AKIIBWA ANAKUWA MZITO KULIKO TEMBO!
Hili nalo, Mawimbi analisimulia kama maajabu mengine ya mbuzi wake, kwamba alishawahi kuibwa mara 3 bila mafanikio kwani wezi hao walimrudisha wenyewe baada ya kuelemewa na uzito wake kama wa tembo. Anasema hata akiibwa kwa kuingizwa kwenye gari huwa mzito.
“Wamejaribu kumuiba mara 3 bila mafanikio. Kuna watu kwa nyakati tofauti walifanikiwa kumuiba na kumuweka kwenye gari lakini walishindwa kuondoka naye kutokana na kuelemewa na uzito.
Kutokana na hali hiyo, walimrejesha wenyewe na kuondoka zao. Kuna mwingine siku moja alikata bati kwenye banda na kutaka kuondoka naye lakini mbuzi alimpiga kwa pembe yule mwizi, asubuhi tukamkuta amepoteza fahamu, nikampa shilingi 2000 kwa ajili ya kwenda kujitibu maana aliumia vibaya,” alisema Mawimbi.
AGONGWA NA PIKIPIKI, AVUNJIKA MGUU
Wiki mbili zilizopita mbuzi huyo ambaye amekuwa gumzo pande hizo aligongwa na pikipiki na kuvunjika mguu wa kushoto mbele.
Mawimbi anasema alimfuata daktari wa mifupa wa Hospitali ya Amana ambaye alimfunga bandeji ngumu ‘P.O.P’.
“Kwa sasa mbuzi wangu hana raha, ana maumivu makali kwani hivi karibuni aligongwa na pikipiki, nikamwita daktari wa mifupa pale Amana, akaja akamtibu kwa kumfunga P.O.P, naamini Mungu atamsaidia kupona,” alisema.
ANAWEZA KUWA MBUZI WA UCHAWI?
Mawimbi anakanusha madai kwamba maajabu ya mbuzi huyo hayatokani na mambo ya kishirikina, bali ni uwezo alionao kutoka kwa Mungu.
“Si mbuzi wa uchawi, ila ni mambo ya Mwenyezi Mungu tu,” aliweka wazi Mawimbi huku akiagana na waandishi.
No comments:
Post a Comment