Friday, November 9, 2012

BASI LA TEAM YA YANGA SC LAVUNJWA KIOO CHA DIRISHA LA UPANDE MMOJA

Basi la Yanga


Na Mahmoud Zubeiry
BASI la Yanga limefanyiwa fujo na watu wasiojulikana, wanaosadikiwa kuwa ni mashabiki wa Simba, eneo la Kabuku, wakiwa njiani kuelekea Tanga.
Baraka Kizuguto, Ofisa tovuti wa Yanga aliye katika msafara wa timu ameiambia BIN ZUBEIRY mida hii kwamba, jamaa aliyerushwa jiwe alikuwa juu ya mti na limepasua kioo, ila halijajeruhi mtu.
Amesema wametoa ripoti Polisi, ingawa hawakufanikiwa kumkamata mtu kwa sababu wahusika walikuwa wamekwishakimbia baada ya tukio.
Yanga iliyoondoka leo alfajiri Dar es Salaam tayari ipo Tanga , imefikia katika hoteli ya Central City, barabara ya Nane na jioni itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.
Yanga iko Tanga kwa ajili mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumapili.
Yanga imepania kushinda mechi hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu, ambayo mzunguko wake wa pili utarejea Januari mwakani.
Yanga ilifanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam jana na wachezaji wake wote wapo vizuri, chini ya kocha wake Mholanzi, Ernie Brandts.
Wchezaji wa Yanga wamepania kuvunja rekodi ya Coastal Union kutofungwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani, Mkwakwani, Tanga katika mechi hiyo.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa niaba ya wenzake mapema wiki hii, Nahodha Msaidizi wa Yanga, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ alisema kwamba wanataka kustawisha uongozi wao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuwafunga Coastal Jumamosi.
Alisema wanajua Coastal ni timu nzuri na wanatarajiwa upinzani katika mechi hiyo, ila ameonya Yanga ya sasa ni tishio na wachezaji wako vizuri ‘ile mbaya’.
“Kwa kweli mimi na wachezaji wenzangu tunamshukuru mwalimu mpya (Ernie Brandts) kwa kutupa vitu vipya na muhimu. Timu yetu imebadilika na kila mtu anaona sasa. Wale Coastal si hawafungwi kwao wale, sasa sisi tutaenda kuwafunga pale pale, tena kipigo kikali,”alisema.
Lakini pia habari za ndani kutoka Yanga zinasema kwamba tayari wachezaji wameahidiwa donge nono iwapo watashinda mechi hiyo.
Wachezaji hao, walizawadiwa Sh. Milioni 15 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC mwishoni mwa wiki katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, uliifanya Yanga iongoze Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 26, ikiwa imebakiza mechi moja ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Caostal Union mjini Tanga, ikifuatiwa na Simba SC yenye pointi 23, ambayo juzi imefungwa 2-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.

No comments:

Post a Comment