Saturday, December 29, 2012

Zanzibar sasa hali ni tete


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifuatana na Pd. Cosmas Shayo wa
Kanisa la Roman Katoliki Jimbo la Zanzibar wakati alipokwenda kutoa mkono wa pole kwa
uongozi kanisa hilo na familia kufuatia tukio la kupigwa risasi kwa Pd. Ambrose Mkenda.
Ni dhahiri kwamba hali ya amani visiwani Zanzibar ni tete, huku viongozi wakitajwa kuhusisha dini katika harakati za kufikia malengo yanayotajwa kuwa na nia ovu.

Viongozi wa dini, wanasiasa na wanazuoni, wanaelezea umuhimu kwa Taifa kudhibiti uhalifu na kuwachukulia hatua kali wahalifu wanaochochea vurugu, ili kulinda na kuendelea amani visiwani humo.

Zanzibar inakabiliwa na kukua kwa vurugu, hujuma na njama za kutekekeza mali na maisha ya raia wasiokuwa na hatia, dalili zikionyesha wazi kuwepo ‘mkono wa wanasiasa.’

MAKAMU WA RAIS ZANZIBAR ANENA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema serikali itahakikisha inawasaka na kuwachukulia hatua za kisheria waliompiga risasi  Padri Ambrose Mkenda, Desemba 25, mwaka huu.

Balozi Seif alisema kitendo hicho kimetoa sura mbaya kwa Taifa na serikali, hivyo kinapaswa kulaaniwa na wapenda amani na umoja wa kitaifa.

“Ni jambo baya na la kusikitisha, tena limetoa sura mbaya kwa Taifa. Serikali haitosita kuachukulia hatua dhidi ya watu waliofanya uhalifu huo,”alisema Balozi Iddi na kuwataka wananchi kuheshimu na kulinda misingi ya amani na umoja wa kitaifa Zanzibar.

Balozi Seif alitoa msimamo huo wa serikali alipokwenda kutoa pole kwa uongozi wa kanisa hilo na nyumbani kwa Padri Mkenda mjini hapa jana.

Alisema SMZ imesikitishwa na kulaani kitendo cha watu hao ambacho kinaashiria uvunjifu wa amani pamoja na kuwaweka wananachi katika mazingira ya hofu isiyokuwa ya lazima wakati Tanzania ni nchi ya amani.

PADRI WA KATOLIKI AWAONYA WANAOWAPOTOSHA WATOTO


Padri Cosmas Shayo wa Kanisa Katoliki, aliiomba serikali kuimarisha ulinzi wa raia wema ili kupunguza hofu iliyotanda mioyoni mwao, kutokana na matukio ya hujuma yanayojitokeza visiwani humo.


Padri Shayo alitahadharisha kwamba hulka mbaya  iliyoanzishwa na baadhi ya watu kuwafundisha watoto wadogo tabia ya kukashifu watu wazima kwa sababu ya utofauti wa kidini, inawajengea msingi wa maisha mabovu watoto hao.

“Watoto wadogo kufundishwa tabia ya kukashifu watu wengine, tuelewe kwamba Taifa halitakuwa na mwelekeo mwema wa jamii yake ya baadaye,” alisema.

Padri Shayo alisema serikali inawajibika kufanya uchunguzi wa kina kufuatia kupigwa risasi kwa kiongozi huyo.

Padri Mkenda alipigwa risasi na watu wawili waliokuwa wamepanda pikipiki majira ya saa 1:45 usiku wakati akitoka kumuangalia mgonjwa katika hospitali ya rufaa ya Mnazimmoja akiwa ndani ya gari wakati akisubiri kufunguliwa geti na mlinzi na hakuna kitu kilichoibiwa baada ya kiongozi huyo kupigwa risasi.

Tukio la kupigwa risasi mbili za shingo kiongozi huyo wa kiroho limetanguliwa na mkasa wa  kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga wakati akifanya mazoezi ya viungo Novemba 6, mwaka huu.

Hata hivyo  hakuna watu waliyokamatwa kuhusiana na matukio hayo. Lakini Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi ikiwemo kuwatafuta watu waliyofanya mashambulio hayo tofauti visiwani hapo.

HAMAD RASHID AINYOOSHEA KIDOLE CUF


Mbunge wa Wawi (CUF) Hamad Rashid Mohammed, alisema Zanzibar itaingia katika machafuko makubwa endapo hakutafanyika jitihada za haraka kukomesha chuki za kidini zinapandikizwa miongoni mwa raia wake.

Alisema hali si shwari visiwani humo, akiifananisha na ‘yai jeteta’ ambalo kupasuka kwake, kunaathiri watu wote.

Hamad alisema kihistoria Zanzibar ni nchi iliyokuwa na watu wenye uvumilivu wa kidini kwa miaka mingi na hakuna aliyetarajia siku moja watu watatengana na kuhujumiana kwa sababu ya tofauti za kiimani.

Alisema matukio ya kumwagiwa tindikali kwa Katibu wa Mufti Fadhili Soraga na tukio la hivi karibuni Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae kupigwa risasi na watu wasiojulikana ni baadhi ya matokeo ya chuki hizo zilizopandwa na wanasiasa.

"Hali ya Zanzibar inasikitisha sana, matukio yote mawili ya kujeruhiwa viongozi wa kidini ni jambo la kulaaniwa kwa nguvu zote na inathibitisha kuwepo kwa watu wanaochochea hali hiyo kwa manufaa yao," alisema Hamad.

Alisema kumekuwepo na viongozi wa kisiasa wanashindwa kukemea hadharani jambo hilo kwa sababu wanahusika kuwashawishi na kuwachochea viongozi wa dini kushiriki vurugu hizo.

"Uongozi wa kisiasa umeshindwa kukemea kwa sababu kuna baadhi ya wanasiasa wanahusika, wakati mwingine wanakwenda kwa viongozi wa dini zote kuchochea, lakini ikumbukwe ikitokea vurugu hakuna atakayepona," alisema.

Mbunge huyo asiyetambuliwa na Chama Cha Wananchi (CUF) alichokitumia kugombea na kushinda kiti hicho, alisema suluhu ya tatizo hilo ni kuanzishwa mjadala wa kitaifa kujadili kuhusu chanzo halisi na namna ya kufikia suluhu ya kudumu.

Pia Hamad alisema hakuna viongozi wenye maoni na nguvu ya kuzuia jambo hilo, kwa vile viongozi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa wanatofautiana kiitikadi.

Katika suala hilo alionyesha kufadhaishwa na msimamo wa viongozi wa CUF kutokuwa na upande wa kusimamia kuhusu Muungano, moja ya madai yanayotajwa kutumika kama kigezo cha kuchochea vurugu visiwani humo.

“Ndani ya CUF kuna watu wanataka Muungano wa Mkataba na wengine wanataka Muungano wa serikali tatu, tofauti na CCM ambao wana msimamo mmoja wa serikali mbili,” alisema.

"Hili ni jambo baya sana kwa viongozi wa CUF kutokuwa na msimamo wa kimaadili, haiwezekani chama kuwa na makundi mawili yenye tofauti ya msimamo, kutokana na hili huwezi kusimamia serikali hata mara moja," aliongeza kusema.

Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alielekeza lawama kwa jeshi la polisi na kusema linafanya kazi kisiasa na kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Profesa Lipumba alisema kama polisi wangefanya kazi kwa weledi na kuachana na kutumika kisiasa, matukio yanayotokea Zanzibar yasingekuwepo kwa sababu wahusika wote wangekamatwa.

Hata hivyo alipinga hoja ya Hamad kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar imeshindwa kutekeleza wajibu wake katika kuidhibiti hali hiyo.

CHUKI ZILIATHIRI UTENDAJI WA TUME YA KATIBA MPYA

Wakati huo huo, imefahamika kuwa kutokana na kuenea kwa chuki za kidini, wajumbe wa Tume ya kutafuta maoni ya Katiba Mpya, wanafanya katika hali ya tahadhari, baada ya kukabiliana na matukio ya kibaguzi.

Vyanzo vya habari vimeieleza NIPASHE Jumamosi kuwa baadhi ya wajumbe wasiokuwa waumini wa dhehebu moja wanaofanya kazi kwenye tume hiyo visiwani humo, wanachukua tahadhari kubwa huku wakishindwa kwenda kwenye maeneo yanayoonekana kuwa na watu wenye msimamo mkali wa kidini.

"Mimi mwenyewe ni muathirika wa mambo hayo, lakini siwezi kuzungumzia sana jambo hilo, tunachokifanya ni kutokwenda sehemu tunayoona kuna dalili mbaya," kilieleza chanzo chetu kutoka tume hiyo.CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment