SUALA la Joshua Mulundi anayetuhumiwa kumteka Dk Steven
Ulimboka, katika Misitu ya Pande, limechukua sura mpya baada ya ubalozi
wa Kenya nchini kuamua kumchunguza, ili kubaini kama kweli ni raia wake
au la.
Balozi wa Kenya nchini, Mtindo Mutiso aliliambia
gazeti hili juzi kuwa amesikia taarifa za Mulundi akidai kuwa ni raia wa
Kenya, lakini kama nchi, itahitaji kujiridhisha kabla haijajiingiza
kumsaidia kwa lolote.
Dk Steven Ulimboka |
Mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa haijulikani yuko
mahabusu gani baada ya kuhamishwa kutoka Gereza la Keko jijini Dar es
Salaam kutokana na ufuatiliaji wa vyombo vya habari, amenukuliwa mara
kadhaa na baadhi ya magezeti (siyo Mwananchi) kwamba hatendewi haki.
Pamoja na madai mengine, Mulundi amekuwa akitaka
Ulimboka apelekwe mahabusu ili amtambue kama kweli alihusika kumteka,
ili haki dhidi yake itendeke haraka.
Dk Ulimboka alinukuliwa na vyombo vya habari
akisema kwamba muda kuzungumzia ukweli kuhusu tukio hilo bado na kwamba
hajawahi kuitwa, ili akutanishwe na mtuhumiwa huyo.
Hata hivyo, uongozi wa Magereza nchini ulisema
kwamba hauwezi kumsaidia mtuhumiwa huyo kwa lolote, badala yake ulimtaka
aandike barua ya malalamiko na kumkabidhi mpelelezi wa kesi yake, ili
ayafikishe mahakamani kwa hatua zaidi.
Juzi Balozi Mutiso alisema kwamba kutokana na
suala hilo kuendelea kuwa na utata hasa kuhusu uraia wa mtuhumiwa huyo,
aliamua kutuma ujumbe kwenda Gereza la Ukonga ambako alielezwa kwamba
mtuhumiwa huyo anapatikana, lakini hakufanikiwa kumwona.
“Mimi nilituma kijana wangu leo pale gereza la
Ukonga, lakini alipofika huko akaelezwa hayupo, eti afuatilie vizuri
chanzo chake cha taarifa hizo mahali alipopelekwa. Nikaamua kukupigia
simu (gazeti) ili tusaidiane kujua mahali alipo,” alisema Mutiso.
Mutiso alisema kutokana na hatua hiyo ameamua
kufuatilia ili kujua madai ya mtuhumiwa huyo kuwa raia wa Kenya kabla
hajajihusisha zaidi na suala hilo.
“Taratibu za kibalozi inapotokea jambo kama hilo,
ni lazima awepo mtu au ndugu atakayemtambua kuwa Mkenya, au kupata vyeti
vyake vya uraia. Lakini hatujapatiwa vyeti hivyo. Kwa hivyo tunataka
kuthibitisha kwanza kama ni Mkenya halafu tuhusike zaidi katika suala
hulo,” alisema Mutiso.
Mutiso alisema leo atafanya uamuzi wa kufika
mwenyewe katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa ama kuandika barua ya kutaka uthibitisho wa uraia wa Mulundi.
“Jumatatu (leo) ndiyo nitawasiliana na wizara ili nifahamu kijana huyo yupo katika gereza gani,” alisema Mutiso.
Wiki iliyopita Kamishna Msaidizi na Msemaji Mkuu wa Magereza, Mtiga Omary alisema jeshi hilo haliwezi kumsaidia chochote, lakini ana haki kuandika barua kwa mpelelezi wa kesi hiyo.
Magereza na Serikali
Wiki iliyopita Kamishna Msaidizi na Msemaji Mkuu wa Magereza, Mtiga Omary alisema jeshi hilo haliwezi kumsaidia chochote, lakini ana haki kuandika barua kwa mpelelezi wa kesi hiyo.
“Siyo jukumu letu kumpeleka Dk Ulimboka akaonane
huko, tunachoweza ni kumpatia nafasi ya kuandika barua ya maombi ya
mpelelezi wa kesi hiyo ambaye pia ataipeleka Mahakamani,” alisema Mtiga.
Mtiga alikuwa akizungumzia taarifa zilizoandikwa kuhusu malalamiko ya mtuhumiwa huyo.
Mtuhumiwa huyo hivi karibuni aliiomba Mahakani ya
Hakimu mkazi Kisutu imruhusu kuonana na Balozi wa Kenya, lakini mahakama
ilikataa ombi hilo na kumtaka taratibu za kisheria.
Inadaiwa kwamba, mtuhumiwa huyo ameshafanikiwa
kuandika barua kama sheria inavyoagiza na kufikisha ujumbe kwa viongozi
mbalimbali wanaohusika akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel
Nchimbi lakini hakuna dalili zozote anazoziona za kujua hatima ya kesi
hiyo.
No comments:
Post a Comment