HII sasa ni jeuri ya fedha. Azam FC ina orodha ya makocha watano inayofanya nao mazungumzo, kati yao Kocha Mfaransa wa klabu tajiri Afrika, TP Mazembe, Patrice Carteron ndiye anayesakwa kwa nguvu zote.
Hadi sasa Azam inafanya mazungumzo ya karibu na Carteron ambaye pia anainoa timu ya Taifa ya Mali.
Wengine ni makocha waliowahi kuinoa Zambia, Dario Bonetti na Herve Renard ambaye ndiye aliyeipa Zambia ubingwa wa Afrika mwaka 2012 na kwa sasa anaionoa FC Sochaux ya Ufaransa.
Wengine ni Diego Gazito aliyeifikisha Mazembe fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia mwaka 2010 na mkurugenzi wa ufundi wa sasa wa Mazembe, Lamine Ndiaye.
Makocha hao wote ni wa viwango vya juu na yeyote atakayetua nchini ataweka rekodi ya mshahara.
Habari za uhakika kutoka Azam ni kwamba viongozi wa Azam sasa wapo katika hatua za mwisho za kukubaliana na Carteron ili ainoe timu hiyo katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Kocha huyo ndiye anayewafundisha Watanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu katika kikosi cha Mazembe.
Azam inajipa matumaini kumnasa Carteron mwenye umri wa miaka 43 kutokana na mafanikio anayoyapata akiwa na Mazembe msimu huu katika Kombe la Shirikisho Afrika na kuifikisha timu hiyo katika fainali ya michuano hiyo.
Carteron aliyewahi kuichezea kwa mkopo Sunderland ya England mwaka 2001 akitokea AS Saint-Etienne ya Ufaransa ameifikisha Mazembe fainali Novemba 23 mwaka huu itacheza na CS Sfaxien ya Tunisia jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mchezo wa kwanza na kurudiana wiki mbili baadaye.
Azam inajipanga kuvunja mkataba wa kocha huyo ambaye alijiunga na Mazembe Mei 22 mwaka huu.
Mawasiliano ya Azam na Bonetti, Renard na Gazito kwa sasa yamesimama baada ya nguvu kubwa kuelekezwa kwa Carteron na Ndiaye.
Makocha wengine Dorian Marin wa Romania, Zdravko Logarusic wa Croatia aliyewahi kuinoa Gor Mahia ya Kenya, Fabio Lopez wa Italia na Patrick Liewig wameiomba Azam iwape kazi waonyeshe mambo mzunguko ujao.
No comments:
Post a Comment