Monday, November 16, 2020

GAME DAY SOCCER LEAGUE: DSQUAD YAIBAMIZA OLYMPIA FC 2-1

Timu ya Tanzania Houston Community maarufu kama DSQUAD jioni ya leo katika viwanja vya Living Stones Church vilivyoko Alvin, Texas imeichapa timu ya Olympia FC kwa mabao 2-1 kwenye mashindano ya GAME DAY SOCCER LEAGUE2020 . Olympia walianza mechi kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika ya 32 kipindi cha kwanza kupitia kwa Angelo Paqueta ambaye alipiga mpira uliompita golikipa wa Dsquad mkongwe Peter Bategeki. Bao hilo lilisimama hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Dsquad wakiwa ndani ya uzi mpya wa Tanzania walikianza kipindi cha pili kwa kasi kubwa huku wakiliandama lango la Olympia kama nyuki na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 75 kupitia kwa kijana wao machachari Iluta Shabani Mbappe aliyepiga mkwaju mkali kutoka mita zaidi ya 40 uliokwenda kugonga mwamba wa juu ya goli kabla ya kuzama wavuni na kumuacha kipa wa Olympia Manuel Pacheco akiwa hana na kufanya.

Dsquad iliendelea kushambulia kwa nguvu na kupata bao la ushindi dakika ya 83 kupitia kwa kijana mwingine machachari Ramadhan Aubameyang Ngolo ambaye aliwachambua walinzi wa Olympia baada ya kupata pasi maridadi utoka kwa kiungo Amini Msisi.

Kwa matokeo hayo Dsquad inapanda hadi nafasi ya 3 kwenye msimamo wa ligi ikiwa imebakiwa na mechi mbili mkononi.

Mashindano haya yataendelea wiki ijayo katika viwanja vya hivyo vya Alvin Community College. Nyote mnakaribishwa.


Tanzania Houston Community DSQUAD
Wakongwe Rahim Chomba Veron na Cassius Pambamaji

From left: Ally Abaenya Ngolo, Ramadhan Ngolo, Iluta Shabani, Cassius na Amini Msisi


No comments:

Post a Comment