Sunday, November 8, 2020

GAME DAY SOCCER LEAGUE: DSQUAD YATOKA SULUHU 2-2 NA WEST CITY FC

Timu ya Tanzania Houston Community maarufu kama DSQUAD jioni ya leo katika viwanja vya Alvin Community College vilivyoko Alvin, Texas imetoka suluhu ya mabao 2-2 dhidi ya West City FC kwenye mashindano ya GAME DAY SOCCER LEAGUE2020 . DSquad walijipatia bao la kwanza katika dakika ya 33 lililofungwa na beki wake wa pembeni Abubakar Mudhihir kwa mkwaju mkali baada ya kupanda mbele kusaidia mashambulizi. West City walisawazisha  bao hilo dakika ya 43 kupitia kwa Espinoza Javier baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa DSquad.

Winga machachari aliyeingia kipindi cha pili Iluta Shabaan aliifungia DSquad bao la pili maridadi kabisa katika dakika ya 47 baada ya kuunganisha pasi safi ya nahodha Rahim Chomba. DSquad waliendelea kulisakama lango la West City na kukosa magoli mengi sana ya wazi kabla ya City kusawazisha katika dakika ya 89 kupitia mpira wa adhabu ndogo iliyopigwa na kiungo wao Pablo Rico iliyokwenda moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa Dido Jagokwambe akiwa hana la kufanya.

Mashindano haya yataendelea wiki ijayo katika viwanja vya hivyo vya Alvin Community College. Nyote mnakaribishwa.


No comments:

Post a Comment